HADITHI FUPI Na. 5
PEMBE CASSAVA PRODUCTS
MTUNZI: ISIHAKA ‘NUKTA’ KIBAO
Ilikuwa saa 10 alasiri, nyuso zote zilikuwa na huzuni zikitafakari safari ya maisha ya mwana Adamu. Huwa hamna lolote, si majigambo wala ukubwa wa mtu, nguvu zake, utajiri, wala umaarufu. Sote safari yetu ni moja, akhera, na kila mtu atapitia mlango wa umauti. Kama sheikh alivyokuwa akimalizia mawaidha pale makaburini ya kuwa kila nafsi itaonja umauti na kwa Mwenyezi tutarejea.
Msafiri, alikuwa rafiki yangu niliyesoma nae shule ya msingi na kupotezana nae kwa muda mrefu, ila kama bahati tu tulikuja kukutana ikiwa mimi nipo kwenye harakati za kutafuta ajira ndipo urafiki wetu ukarudi kwa kasi kwani yalipita mengi na tulikuwa na mengi ya kufanya ili tuyajenge maisha kupitia mipango ya miradi tuiyoiweka. Msafiri alikuwa msomi wa kiwango cha degree, tofauti na mie nilieishia kidato cha nne na kusomea udereva. Ila ilikuwa kazi ya mungu na hatimaye ametangulia mbele ya haki na kuniacha njiani. Nilijiskia uchungu kwa kuwa alikuwa rafiki na mwenzangu kwenye mipango tuliopanga.
Baada ya mazishi watu walitawanyika wakiwamo Baba Mzazi wa Msafiri, nilimfuata na kumpa pole yake na kumsihi kuwa mvumilivu kwenye kipindi hiki kigumu. Alinitazama usoni na kunishukuru ila hakuweza kunitambua kwa haraka kama tulikuwa tukicheza wote na mwanawe kipindi tuko wadogo nyumbani kwake. Ila sikutaka kumkumbushia maana haukuwa muda muafaka. Nilitoka maeneo yale ya makaburi ya Kinondoni na kuelekea nyumbani Gongo la Mboto huku nikifikiria nafanyaje mipango ile kwani Msafiri kwa kiasi kikubwa ndio alikuwa mtoaji hela kwenye mipango yetu.
Nililala huku nikiwaza nitafanyaje niweze kuboresha maisha yangu kwani hata ajira niliyokuwa nayo nilishikwa mkono na kuwekwa kwa mchango wa Msafiri. Sasa ameshafariki, isije ikawa ameondoka na nia za watu kutaka niendelee kuwepo kazini, nilipiga moyo konde na kuendelea na kazi. Kulipokucha nilidamka kama kawaida na kuelekea kazini, niliwahi sana kuliko siku zote hadi mlinzi wa ofisini akanishangaa na kuniuliza
“Leo kulikoni?”
Nikamjibu, “Jana sikulala vizuri kwani nilikuwa natafakari mengi”
Yule mlinzi alinielewa kwani tulikuwa marafiki wa karibu kiasi chake. Hivyo akanipa moyo na kunieleza nisiwaze sana wala kukata tama na niendelee kupiga kazi kwani mtoaji riziki ni Mwenyezi pekee.
Mazingira yangu ya kazini kiukweli hayakuwa endelevu kwani kila siku zilivyokuwa zikiyoyoma mahusiano na wafanyakazi wenzangu yalikuwa yakipungua taratibu kama mwendo wa kuzama jua. Nililiona mapema, kwa kuwa ofisi ilikuwa ni ya watu asili ya bara Asia, hivyo alikuwa anaandaliwa mtu wa kuchukua nafasi yangu.
Hatimaye baada ya miezi mitatu nikaja kupewa barua ya kuwa ofisi inataka ipunguze baadhi ya wafanyakazi kwani gharama za uendeshaji zimekuwa kubwa na hivyo ikanibidi mimi niwe mmoja kati ya wanaotakiwa kuondoka katika nafasi ile. Siku nakabidhiwa ile barua, moyoni mwangu sikujaa hofu kwani nililitarajia lile na nilikuwa nikiomba mungu aniandalie mazingira mapema ya kujikwamua kiuchumi, kwa hivyo nikawa katika mtihani wa subira maana kwengine kote kulikuwa hakuna mang’azo.
Niliipokea barua, nikapumzika na kazi ile ila nisingependa kuitaja ofisi kwa jina. Nilipitia kipindi kigumu sana katika maisha yangu kwani ilifikia kipindi ilikuwa sina hata nauli ya kuja mjini kutafuta kazi kutokea kwangu Gongo La Mboto. Kwa bahati, nilikuwa nimelipa kodi ya mwaka mzima kwa msaada wa Msafiri, aliniongezea fedha kidogo katika chumba nilichokuwa nakaa, hivyo pakuweka ubavu nilikuwa napo kwa muda. Ilipita miezi saba, kula yangu ya mashaka, sikuweza kununua hata nguo wala viatu vipya na michango yote ya kijamii ikiwamo harusi, misiba na mengineyo watu waliniona mchungu. Ilikuwa nafanya vibarua tu na “Udeiwaka kwenye magari”
Ndipo siku moja nilikuwa natokea zangu Ukonga narejea nyumbani, katika katika pita pita zangu kwa mguu nikaamua kwenda kibanda cha magazeti, naikumbuka siku hii kwani pale ndipo nilipopata msingi wa mabadiliko ya maisha yangu na mpaka kuwa hivi nilivyo. Nilikuwa sina hela ya kununua gazeti, hivyo nikapitia vichwa vya habari magazetini na nikaishia kuondoka, wakati naondoka eneo lile likanipita basi la abiria likiwa linaelekea Chanika likitokeaaaa…. Buguruni kama sikosei. Lile basi lilikuwa linakwenda kwa mwendo wa taratibu huku likivizia abiria kwani wengi ilionekana walishuka pale Ukonga.
Nikalitazama kwa makini huku likiendelea na safari yake, kwa nyuma ya lile basi nikaona msemo umewekwa “Lipo linaloshindikana Chini ya Jua – Kupiku ufanisi wangu”. Ule msemo ulinishangaza na kunishtua, nikatabasamu kwani niliona ni ubunifu wa maneno tu. Lakini wakati naendelea na safari yangu, ule msemo ukanirejelea kichani na kunifikirisha kidogo, hivyo nikawa najiuliza. Yulemwandishi alimaanisha nini? Chini ya jua… ufanisi… nilitafakari kwa muda na kuja kugundua kuwa unapokuwa mahiri kwenye jambo Fulani na ukalifanya kwa ufanisi basi hakuna atakaeweza kufanya kama wewe.
Aaaah! Nikamkumbuka Msafiri rafiki yangu, nikatembea haraka haraka hadi kufika nyumbani na kufungua yale makaratasi tuliyo andaa kwenye mikakati yetu na kugundua kuwa, mipango yote ilikuwa mimi ndio mtendaji mkuu maana wazo la biashara yetu nililitoa mimi kutokana na uzoefu wangu wa biashara ile, Msafiri alikuwa ni mtoaji mtaji mkuu pamoja na kujitolea baada ya muda Fulani kwani biashara za usafirishaji alikuwa hazifahamu kabisa.
Niliamua kupitia upya ule mpango mkakati na kutafakari nitapataje mtaji wa kuanza biashara ile. Likanijia wazo la mkopo kwenye taasisi za fedha lakini halikuwa wazo zuri kwani ndio nilikuwa naanza biashara hivyo ingekuwa hatari kwangu, nikaangalia nani wa kumfuata ili aweze kunikopesha fedha, ila pia ilikuwa ngumu kwa maana kila niliemfuata aliniona ni mtu ambaye sina uhakika wa kurudisha zile fedha. Hivyo ikanichukua muda mrefu kiasi nikafikiria kuachana nalo tena lile wazo.
Siku moja jioni nikiwa nimekaa, likanijia wazo jingine, nikajisemea kwa nini nisimfuate Baba yake Msafiri nimuelezee nini tulipanga na mwanae na tulifikia wapi, ila akili nyingine ikawa inapingana na wazo lile kwani isije ikawa Mzee anaona nataka kutumia jina la mwanae kupata fedha kutoka kwake, na nikiangalia hata mwaka haujatimia toka mwanae afariki. Lakini nikapiga moyo konde nikasema nitamfuata kwani mguu wa kutoka Mungu huutia Baraka.
Asubuhi yake nikatoka na kuelekea nyumbani kwa Mzee wake Msafiri, nilipofika haikuwa kazi rahisi kwani niliona vigumu mwanzoni kumuelezea ila nikawa sina budi na kumueleza ya kuwa mimi na mwanawe tulipanga kufanya biashara ya usafirishaji bidhaa, tukianza na mchele kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam na kisha kusafirisha mihogo kutoka Tanga kuja Dar es Salaam. Ila tulikuwa hatuna usafiri wa kwetu wala ofisi ya biashara, na kwa kiasi kikubwa mtaji aliahidi kutoa Msafiri ili nami niingize nguvu kazi kwani nina uzoefu wa mambo ya usafirishaji.
Nakumbuka Mzee wangu huyu aliniuliza, kwa nini tulitaka kufanya biashara ile. Nami nikamjibu, kujikwamua kiuchumi na hatimaye kuwa na kitu cha kwetu cha kujivunia kitakacho tuwezesha kusema “Sisi tumefanikisha haya, na tunamiliki hiki na hiki”. Mzee alinisikiliza kwa makini melezo ya biashara ile na alivutiwa sana kwa vile tulivyokuwa tumepangilia ile biashara na vile itakavyokuwa inaenda. Baada ya kumaliza kumuelezea mchanganuo wa biashara, alitabasamu na kunifanya nijiskie kama mtu aliepumzika kivulini kutokana na kupigwa na jua kali na kuhisi kuna matumaini.
Akanambia, sikiliza mwanangu ‘Mimi ni kama Mzee wako, ulivyonikumbusha kipindi mnacheza wote na mwanangu kipindi wadogo nikakumbuka vitu vingi kuhusu mwanangu. Na kama ndoto hii mwanangu alitaka kuitimiza, mimi nitakusaidia kwani nafahamu hata yeye atafurahia huko alipo’. Nakumbuka pia aliwahi kunigusia kutaka kuanzisha biashara ila hakunieleza kinaga ubaga kutokana na safari zangu kikazi. Mzee akaniahidi kunipa mtaji wa milioni 3 ili nianze biashara ya kusafirisha mihogo kutoka Mapojoni, Tanga na kunambia kule Tanga pia ana marafiki zake ataniunganisha nao ili biashara iende kwa uhakika.
Nilitabasamu na kumshukuru sana Mzee kwa shukrani zote kwani alikuwa amempiga teke chura, na nikamuahidi sitomuangusha kwa mchango wake ule. Zilipita siku kadhaa, akanikabidhi mtaji ule, nikawasiliana na marafiki zake wa Tanga kupitia jina lake, wakawa wananikusanyia mzigo namimi kuupokea Dar es Salaam kwa kuusambaza. Biashara ilikuwa ya mafanikio makubwa sana kwani niliweza kuchukua mzigo mwingi na hatimaye kuwa na usafiri wangu wa kuchukulia mzigo Tanga, nikamiliki ofisi ya usambazaji na mwisho nami nikaajiri watu wawili.
Nimefikia hapa, ni miaka mitatu sasa ambayo ni ya mapito aina mbali mbali lakini kitu kilichokuwa kinanipeleka mbele kwanza ni ule msemo “Lipo linachoshindikana chini ya jua – kupiku ufanisi wangu” kwani nilijitahidi kwa hali na mali kuhakikisha nabaki kwenye biashara na nazidi kukuwa kimafanikio, Baba yake Msafiri yeye ndiye alikuwa ufunguo wa safari yangu hii, kwani ukiachilia mbali kunichukulia kama mwanawe, aliniamini na kuthubutu kuweka pesa yake kwenye biashara hii nami sikumuangusha kwani amejionea ninachofanya na mpaka sasa amekuwa mdau mkubwa na msimamizi mkuu wa PEMBE CASSAVA PRODUCTS.
Mpaka nafungua kiwanda cha kati na kati kiuzalishaji ni mashauri yake Baba Msafiri na hekima zake juu ya uendeshaji wa biashara na usimamizi. Hakuniacha Mzee wangu huyu nami bado naendelea kuchota hekima kutoka kwake. Mafanikio niliyoyapata kuanzia kumiliki usafiri wa biashara, usafiri binafsi, kuwa na makazi nyumbani hadi kujenga familia ni chachu iliyotokana na biashara hii na Mzee wangu huyu.
Hivyo ningependa niwashukuru kwa kusikiliza historia yangu kwa ufupi naamini itaweza kushawishi vijana wenzangu na jamii kwa ujumla. Mwisho ningependa muendelee kutumia bidhaa za PEMBE CASSAVA PRODUCTS kwani ni bidhaa bora sokoni, kuanzia unga wa muhogo, mihogo, na miche kwa ajili ya kupandia.
-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
“Naam, huyo ndio bwana Mwinyipembe Mzava, Mjasiri Wa Mali wetu wa leo, umekuwa ni mshawishi mkubwa kwa vijana na kwa hakika umetuletea mapinduzi ya kifikra na kiuthubutu, kwani historia yako itawaathiri watu wengi leo”
Aliongea Fatime, mtangazaji wa Nukta FM, radio ya Tanga. Aliongeza, “Tunakushukuru Bwana Mwinyipembe kwa kuwasili kwenye kituo chetu cha radio Nukta FM na kuridhia kuelezea historia yako ya maisha tokea ulipoanzia mpaka hapa ulipo. Kwani ni kijana mwenye mafanikio ya kuigwa na tunaamini utaendelea kushawishi wengine kwa vitendo na maneno, taifa letu linahitaji kujua watu kama nyie mlianza vipi na mlipita pita vipi ili watu wapate funzo na wachukue hatua. Hilo ndio lengo kuu la kipindi chetu cha MJASIRI WA MALI.”
Baada ya hapo Fatime alimalizia kwa maneno machache
“Nawashkuru watu wote waliotega sikio kwenye kipindi chetu cha leo na kusikiliza historia fupi ya Msajiri Wa Mali Bwana Mwinyipembe, kwani naamini tumejifunza mengi na tuendelee kupambana. Unapokuwa na wazo lako usikae nalo tu, jaribu kutafuta nani wa kumfuata ili uweze kuwezeshwa kwa namna moja au nyingine. Endeleeni kusikiliza Nukta FM kwa vipindi vijavyo, endelea kutega sikio”
Fatime alinigeukia na kunipa mkono wa shukrani kwa kuwasili kwenye kipindi kile kwani niliweza kushawishi wachangiaji wengi kupitia ujumbe mfupi wakati wa mahojiano yale, na wengi walikuwa vijana wakitaka tuonane kwa ajili mashauri ya biashara. Tuliagana na Fatime nami nikaweza kuchukua usafiri wangu ambao nilikuwa nimeenda nao na kuelekea nyumbani kwa nilikuwa nahisi njaa na nilipofika nilimkuta mke wangu kashaniandalia chakula kwa ajili ya kula.
MWISHO
****************************************
HADITHI Na. 4:
JINA - "SALMA"
MTUNZI : ISIHAKA 'NUKTA' KIBAO
Yalikuwa matone ya damu yakinimwagika kwenye mkono wangu mithili ya bomba la maji ambalo halijafungwa mpaka mwisho, sikuweza kuinuka kwani sikuweza kabisa kuinua miguu yangu. Kila nikiitazama na kujitahidi kuiinua naona kana kwamba miguu ile si yangu. Sikuweza kufanya chochote. Kwa mbali nikasikia watu wakipiga yowe huku wakielekea upande nilipo.
“Ajaliiiiii… njoooni huku, pia kuna watu”
Sauti ile, yasemekana ilikuwa ya ukali na ya nguvu lakini kwa upande wangu ilikuwa ni sauti yenye kufifia na kutoskika vizuri. Sikuweza hata kumjibu mwana mama yule ambaye alikuwa na nia ya kunisaidia eneo lile. Nikashkuru kwa kelele zake kwani niliishia kuona kundi la watu likinizunguka kwa idadi kuongezeka huku mie macho yangu yakiishiwa nguvu na kufumba. Nikapoteza fahamu.
Baada ya muda nafumbua macho na kuangaza kila pembe pale mahala nilipo nikagundua nimelala kwenye kitanda chenye maandishi makubwa “MSD”. Nikajiuliza katika akili yangu na kugundua niko hospitali kwani harufu za dawa na wagonjwa wengine kwenye vitanda vingine nao pia walikuwa wakinitazama. Wengine kwa mshangao, wengine kwa kutokujali na wengine waliendelea na shughuli zao.
Kitanda cha pembeni yangu nilichokuwa nimelala alikuwa amelala kijana mmoja, rika langu, nikamtazama na kumuangalia vizuri nikaona amekatwa mguu mmoja. Nikajiangalia na mie nikaona miguu bado ninayo ila siwezi kuisogeza, nikamuita na kuanza kuongea nae.
“Habari yako”
Akanijibu “safi”
Nikamuuliza “hapa ni wapi?”
Akanijibu “Hapa ni Tumaini Hospital”
Akanitazama kwa dakika kadhaa na kuniambia
“Unajua sisi binadamu tunajidai sana na kujisahau hali ya kuwa kabla hatujafa hatujaumbika, kwa maana ulivyoletwa juzi ulikuwa huna fahamu kabisa. Tukajua wewe ni safari, hutaamka. Ila ushUkuru sana, Mungu kakurudisha tena, unapaswa kumrudia kwa nguvu zako zote rafiki yangu”
Alivyonambia vile, nikajiinamia na kuvuta kumbukumbu mara ya mwisho nilikuwa wapi. Mbali na kile alichonambia, akili yangu ikawa inawaza miguu yangu tu, kwa nini siwezi kuinuka. Baada ya muda kidogo nikamuona Salma anakuja na daktari huku wakiwa na kiti cha magurudumu “Wheelchair”. Nikashtuka sana nikajisemea,
“Mungu wangu ndio nimeshakuwa kiwete? Itakuwaje? Maisha yangu yatakuwaje? Malengo yangu je?"
Yakanijia maswali mengi sana kichwani mwangu ila kabla sijaendelea na mawazo yale, Salma na Daktari wakawa wameshafika pale kitandani kwangu.
Salma alikuwa ni msichana mwenye upendo wa kweli sana, alinipenda bila ya kujali tabia yangu ya ujana kwa kupenda starehe za pombe, muziki na ulevi wangu mwingine mkubwa wa mapiki piki. Alikuwa kila siku akinisihi niache tuyajenge maisha ila sikuwa nampatiliza. Salma kwao walikuwa ni watu wenye uwezo sana wa kifedha kwani baba yake alikuwa Balozi mstaafu. Hivyo pesa haikuwa ikiwapiga chenga.
Alinifuata karibu yangu na kunisalimu,
“Habari Zaki, Umeamkaje leo?”
Nikamuitikia Salamu kiunyonge na kumwambia “Nashkuru nimeamka salama. Nina uchovu mwingi tu”
Salma aliniangalia usoni kisha akaitazama miguu yangu, alijua nilichokuwa nakitarajia kutoka kwake kuhusu maelezo ya Daktari maana uso wangu ulikuwa na maswali yote ambayo yalijionesha bila ya kutamkwa na kinywa.
Salma aliendelea kuongea, “Zaki,nilipigiwa simu na Melanie, alikuwa karibu na tukio la ajali uliyopata na kunieleza kilichotokea na wapi ulipelekwa. Usijali, kwani nilikuwa nikikusimamia tokea juzi, na sikukata tamaa kwani nilijua utaamka ijapokuwa nilijawa na hofu juu ya hali yako. Nilimuomba sana mungu usiku kucha na namshkuru kwani dua zangu alizijibu”
Nikamtazama usoni na nikamuita “Salma, nashkuru sana kwa yote ulionifanyia, sina la kukulipa. Ila miguu yangu, siwezi kuisogeza.”
Nikamgeukia Daktari, “Dokta, miguu yangu vipi? Nitafanyaje kazi zangu, maisha yangu yatakuwaje?”
Daktari alisogea karibu na kunishika bega, kisha kunambia
“Zaki, pole sana. Ulipata ajali mbaya ya pikipiki na tunashkuru umeweza kupambana umerudi leo uko nasi tena, tumefanya uchunguzi wa awali kuhusu miguu yako. Kwa bahati daktari wetu bingwa alikuwepo jana usiku, anaehusiana na mishipa. Kwa mujibu wake anasema utakuja kutembea na kuendelea na shuguli zako kama kawaida. Ajali uliyopata imesababisha baadhi ya mishipa yako ya fahamu kuminywa na kupeleka mawasiliano hafifu kuendea hakuna kutokea kwenye uti wa mgongo kuelekea miguuni kwa sababu pingili za uti wa mgongo zimeshtuka na kusababisha hayo.
Unapaswa kutumia dawa na mazoezi ya viungo ili urudi kwenye hali yako ya kawaida. Itakuchukua muda ila utapona, ni juhudi tu, bila ya kukata tamaa.”
Kwa maneno yale, nikajisikia vibaya kwani ajali ile ilikuwa ni sababu ya mwendo kasi wangu. Hivyo nilijitakia mwenyewe, lakini maelezo yale ni kama yalikuwa kinyume kwa Salma kwani alitabasamu na kunishika mkono na kunambia.
“Zaki, daktari ametuthibitishia kuwa utatembea. Kwa hivyo kwa sasa ni dawa na mapumziko ya kutosha”
^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^
Baada ya mwaka kupita sikuamini kama ningeweza kukunja goti mbele ya Baba Mkwe mtarajiwa huku Sheikh pembeni akitushikisha mikono na kututamkisha maneno ya kufunga ndoa baina ya mimi na Salma. Salma alinitoa mbali, nilikuwa nikimdharau, kutokumjali na kuutesa moyo wake. Ila alipigana na hali yangu mpaka nikaweza kutembea tena, alikuwa akija nyumbani kila tarehe ya mazoezi ilipokuwa ikifika na kunichukua kunipeleka hospitali na kunirudisha.
Moyo wake wa ajabu ulinitia nguvu na nikatia nia kurejea kwenye hali yangu ya kawaida. Ilikuwa kila nikimtazama sioni cha kumlipa zaidi ya nami kumzawadia moyo wangu ambao alikuwa akiulilia miaka nenda miaka rudi. Salma kwangu-kwake nilikuwa kama vile penye miti hakuna wajenzi, ila nilikuja nikalitambua hilo na kumkubali ikiwa pamoja na kumpa moyo wangu. Hivyo baada ya ndoa tuliweza kujenga familia na tukaishi vizuri pamoja na kupata mmoja.
MWISHO
***************************************
HADITHI FUPI FUPI Na. 03
Nilikuwa napiga hatua kidogo kidogo huku nikiwa sijali vumbi wala vijiwe jiwe vilivyokuwa vinaniumiza wakati nikivikanyaga huku viatu vyangu vikichafuka kwa vumbi la mwendo mrefu, pamoja na fujo za mtaa ule za watoto kucheza mpira wa miguu huku wakiwa wamechimbia miti ardhini kama magoli, wanawake upande wa pili wakiwa wamejikusanya wakisukana wakiwaonya wale watoto kutowapiga na mpira, wengine wakiendesha baiskeli kwa kufanya njonjo lakini akili yangu yote haikuwa katika mazingira yale.
Kilichokuwa akilini mwangu ilikuwa ni mawazo ya harusi ya msichana Belinda. Kwanini imepita kwa mtindo ule, na kwanini alinifanyia vile? Nilijiona ni kiumbe nisiye na thamani pale mjini. Mtaa ule wa fujo niliweza kuupita kwa huruma ya Mungu kutokana na fujo zake kwani nilikuwa mfano wa kivuli kiasi watu kutonijali wala kunigonga na aidha mpira au baiskeli za watoto.
Baada ya kuuvuka mtaa ule salama salmini nikamkumbuka Shukuru ambaye alikuwa ni kaka wa Belinda. Nikaingiza mkono mfukoni na kutoa simu ili nimpigie, kwani yeye ndiye angeweza kunipa maelezo stahiki ya harusi ile. Mara ghafla nikaona gari imepita kwa kasi huku ikiuelekea mtaa ule wa fujo. Nikajiuliza ni nani awezaye kuendesha kwa fujo namna ile kwenye mitaa iliyojaa watu, haikupita dakika moja nikaskia kishindo na makelele ya akina mama. Mawazo yote yakaniruka na ikanibidi kuelekea kwenye eneo la tukio kushuhudia nini kinaendelea.
Kwa kuwa sikuwa mbali nikafika pale mara moja na kuona watoto na wale akina mama wamezungukia kitu katikati, akili yangu ikanipa ni ile gari imesababisha ajali mahala pale. Sikuwa mbali na ukweli kwani ilikuwa ajali na mtoto wakiume mmoja alikuwa amegongwa. Baada ya kuona vile nikafanya haraka kuingia katikati ya kundi lile na kutoa msaada kwa kumpatia yule mtoto huduma ya kwanza na kuwaamuru wasogee mbali kidogo ili mgonjwa apate hewa safi kwani alikuwa amelala chali na damu zikimtoka upande wa sikio la kushoto.
Kuangalia kwa pembeni, aliyesababisha ile ajali alikuwa ni kijana mdogo ambaye alikuwa ameshikwa na butwaa asijue la kufanya, maana watu walimzonga huku wakimzogoa. Mara akatokea mtu mzima mmoja wa kiume ambaye alijulikana kuwa ndiye mzazi wa yule mtoto, akiwa na wasiwasi mkubwa juu ya hali ya mwanae. Ndipo nikamueleza kuwa Mimi ni Dokta na yambidi afanye haraka kumuwahisha mtoto hospitali. Yule aliyesababisha ajali ikambidi abebe jukumu la kumpeleka mtoto hospitali, nami baada ya kuona hali ile ikanibidi niingie garini ili nikatoe msaada zaidi.
Tulifika Hospitali ya Rufaa ya Bombo (Tanga) saa moja na dakika tano usiku. Nami nilivyoingia pale, muuguzi Maria baada ya kuniona tu akanisalimu
“Dr. Kera, kwema? Mbona umerudi uko hai hai…”
Nikamwambia
“Nina mgonjwa na yambidi niingie nae chumba cha watu mahututi”
Hivyo akafuatilia kitanda mara moja cha kumbebea mtoto yule, huku mimi nikienda chumba cha madaktari kujiandaa ili kuokoa maisha ya mtoto yule. Tunaingia chumba cha watu mahututi ni saa moja na dakika ishirini na tano.
Tunaanza uchunguzi wa mgonjwa yule, kitu cha kwanza tunagundua damu nyingi zimemtoka sikioni na kwa upande wa uchogoni inaonekana kuna ubonyeo kana kwamba alijipigiza na uchogo alivyoanguka. Baada ya uchunguzi huo wa awali, namwagizia mhudumu Rukia alete mashine ya kupumulia ndipo tunagundua mgonjwa wetu yule hapumui tena kwani mashine ile haikufanya kazi, anakata pumzi na kufariki.
Tukafanya juhudi zetu za kumuokoa kwa kuushtua moyo na kumsugua kifuani ila haikufaa. Baada ya kuona vile nikarudi hatua moja nyuma na kuangalia saa, nikaona ni saa moja na nusu.
Nikafikiria itakuwa ngumu kiasi gani kwa mzazi wake kumpa habari ile, ila nikapiga moyo konde kwani madaktari ni sehemu ya kazi yetu kutoa habari za msiba kwa wahusika na nikafanya hivyo. Nikamueleza baba wa mtoto habari ile na niliushuhudia uchungu wa mtoto kwa mzazi ila ndio ilikuwa kazi ya Mungu.
Baada ya pale nikaona nijiwekeze zaidi kwenye kazi yangu na kuachana na habari ya Belinda kwani usaliti alonifanyia haukuwa wa kawaida kuchukuliwa na rafiki yangu wa karibu kipindi niko masomoni nje ya nchi.
MWISHO
HADITHI FUPI FUPI
HADITHI Na. 02
JINA: MPELEKESHA MAUNGO
Yalikuwa macho
yake kama vile anaeniangalia muda wote, ni kama vile mtu alie na kifaa cha
kuupelekesha moyo wangu kwani kila akisogea basi huuamuru moyo wangu na kuanza
kudunda kwa kasi isivyo kawaida. Na pale anaponisogelea hata kama ni kwa bahati
mbaya iwe kunisalimia au kuongea chochote basi miguu yangu huhisi mizito na maneno kuniishia.
Hali hii ilikuwa
haizoeleki kabisa na kila siku nilikuwa nasema na nafsi yangu mpaka ikafikia
mahala nikasema laiti kama nyie viungo vyangu mna midomo basi ningewauliza ni
kwa nini mnanikosesha raha namna hii ila ndio havina midomo, kwa hivyo mateso
yalikuwa pale pale. Siku moja naelekea zangu darasani nikasema leo napigana na
hii hali kwani haiwezekani mateso haya yanipelekeshe.
Mwili wangu
mwenyewe lakini unanipa tabu na anaenipa tabu nakutana nae kila siku, ulipofika
muda wa mapumziko mara nikamuona “Mpelekesha Maungo” yangu anakuja na kundi la
wenzie, nilimtunga hivyo kutokana na mateso anayonipa, nikajisemea leo namaliza
hii hali na kuhema.
Alipokuwa anakuja na wenzie, kwa mara ya kwanza mdomo nao
ukanisaliti kwani kila nilipotaka kumuita nikajikuta nasita, na kujitungia
sababu ya kuwa anaweza kukasirika kwa kuwa namuita mbele ya hadhara ama
nitamkatisha safari yake, nikajiruhusu kupoteza nafasi ile na kujipa moyo kwa
nyingine.
Nikaiambia akili
yangu ya kuwa leo nimeshindwa ila sitajiruhusu baadae akiwa pekee kwani
nitamkabili na kuuamuru moyo wangu ujaze ujasiri wa kuzungumza hisia zangu ili kuziweka wazi na kuona nini kitatokea. Ilipofika jioni wakati narejea zangu
nyumbani huku nikipiga hatua taratibu taratibu mara ghafla kwenye kona ya kuelekea nyumbani
namuona Mpelekesha Maungo yangu.
Roho ikanipasuka kifuani na mara hii ni kama moyo umefungwa injini ya magari ya
mwendo kasi, Mpelekesha Maungo huyu hapa mbele yangu.
“Mambo”
alinisalimia
Nikaitikia “Poa”
Nikamuuliza
“Mbona uko mitaa hii…? ahhh ah, yaaaani huwaaaaa sikuoni maeneo haya.”
Ukimya ulitawala
kidogo kama sekunde kadhaa hivi, kana kwamba alikuwa alikuwa anafikiria jibu.
Nikaona kama nimekosea kuuliza, nika mtazama usoni.
Basi nikasikia kuna kijisauti katika akili yangu kikinambia
“Shika mkono
wake muongozane nyumbani…..”
Kabla kisauti
kile hakijamaliza shauri akainua macho na kunijibu, “Nimetoka pale kwa rafiki
yangu”
Kale kasauti
kakarudia shauri lile na nikajikuta namwambia “Mimi naishi pale mbele”
nikamuonesha kwa kidole. Huku kiroho kikinidika dika, ila safari hii nikajikaza
na kumwambia “Karibu ukapaone”
Akanambia “Sawa”
Nikashusha pumzi
kwani sikuamini kama angesema vile, ndipo tukaongozana na kumfikisha pale
nyumbani ninapokaa.
^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^
Mara nasikia
simu inaita, kuangalia ni Mama Zai, nikapokea kwa haraka kwani nilitaka kujua nimeandaliwa nini nyumbani.
“Mama Zai, bora
umepiga mke wangu. Kuna nini leo nyumbani? Kuna haja ya kupitia sokoni?”
Mama Zai
akanijibu “Hapana mume wangu, njoo tu nyumbani tumeandaa kile chakula
ukipendacho”
Nikamwambia "Sawa mke wangu, ndio natoka kazini. Muda sio mrefu ntafika nyumbani" Nikaikata
Baada ya kukata simu,
Frank rafiki yangu niliekuwa nae kwenye gari ndogo tukitokea kazini, akacheka
na kuniuliza,
“Kwa hiyo huyo
ndie yule Mwendesha Maungo yako?”
Nikamwambia
“Ndio, tena amekuwa mtawala wa maungo na si mwendeshaji tu… kapanda cheo. Sasa
hivi ni Mama Zai”
Frank kwa sauti
ya kicheko akasema “Aisee mmeanza mbali, hongera rafiki yangu. Utakuja
kunimalizia hadithi siku nyingine unambie jinsi ulivyotetemeka kusema hisia
zako”
Wote tukacheka
kwa nguvu na kuendelea na safari, hatimae nikamuacha njiani Frank karibu na
mitaa ya kwake nami nikaelekea nyumbani.
MWISHO.
******************************************
HADITHI FUPI FUPI
HADITHI Na: 01
JINA:
PEMBA - DAR
“Kimya ndo kilikuwa mfalme wa
chumba tulichokuwemo na kama utulivu ungekuwa na roho basi ungekuwa shahidi kwa
kutoa ushuhuda wa nyuso na hisia za watu zilivyoshikwa na mshangao kwa muda wa
takriban dakika kumi.
Haikupaswa kutokea yaliyotokea kwa
yule Mzee, alikuwa akipendwa na watu wa rika zote. Bashasha na uaminifu wake
ndivyo vilikuwa viungo muhimu alivyotumia kuunganisha familia, majirani na
jamii kwa ujumla. Ugomvi, hasira na maachukizo kwake vilikuwa miba na sumu
kiasi aliweza kuving’oa na kumimina busara katika maamuzi aliyokuwa
akiyachukua.
Hakuwa na mbwa katika mji wake
kiasi ajilinde na uwizi wa vibaka na majambazi. Ila nyumba yake ilikuwa
yajulikana kwa kuonekana hata ukiwa mbali kwa mtaa ule alokuwa akiishi kwa
rangi yake ya indigo. Yasemekana mkewe ndiye aliyependezewa na rangi ile
kupakwa kwenye kuta za nje….”
“Haaaa”,
Mshangao wa jirani yangu nliyekuwa
nimekaa nae kwenye viti vya dirishani ulinikatisha hadithi nlikuwa nikiisoma
kwenye safari yetu na kumuuliza nini tatizo?
Akaniuliza “Inamaana husikii?”
Alivyoniuliza vile ilibidi
nisikilize kwa makini. Mara nikawa naskia “Tuk tuk tuk… tuk tuk.”
Nikamuuliza “Ni nini hiko?”
Akanambia “Hiyo ni mashine na boti
yetu inaelekea kusimama katikati ya bahari”
Nilishikwa na bumbuazi maana sikuwa
ni mtu mwenye kuweza kuogelea. Kila nikiangalia abiria wenzangu naona wengi
wanaomba Mungu na wengine wakiwa na Biblia na Misahafu huku wakisoma dua ila
mimi nina kitabu cha hadithi mkononi. Nafsi yangu ikajilaumu kwa kutobeba
kitabu cha Mungu.
Tafrani zilidumu ndani ya kumi na
tano na baada ya hapo nahodha wa msafara akaja mbele yetu na kututoa mashaka
yakuwa safari yetu itakwenda salama na tusiwe na wasiwasi kwani kulitokea
hitilafu kidogo na sasa imetatuliwa. Hapo ndipo kitabu changu cha hadithi
nikakiweka pembeni na kuanza kumuomba Mungu mpaka nilipofika Dar Es Salaam
nikitokea Pemba.
Utamu unakolea na hadithi ndo yaisha.. Saf sana bro.
ReplyDeleteShukran. Utamu utarudi tena, usitie shaka
ReplyDeleteThis comment has been removed by the author.
ReplyDeleteMbona Umepotea @maryam Albuhry
Delete