Wednesday, 21 February 2018

Historia ya Hayati Salim Ali Kibao

Salim Ali Kibao katika Ulimwengu wa Kiswahili.


              


Salim Ali Hemed Kibao alizaliwa katika kijiji cha Mnyanjani, Mkoani Tanga tarehe 20/10/ 1933. Alipata elimu yake katika shule ya serikali Tanga toka mwaka 1943 – 1945. Na kuweza kusoma masomo ya dini hadi kuhitimu kusoma kitabu cha Qur’an, pamoja na kusoma vitabu vya kujuwa mambo yanayomlazimu Muislamu kuyajuwa kama faradhi, Sunna, haramu na halali n.k. Baada ya hapo alijiingiza kwenye kazi ya ufundi wa kushona nguo kwa kutumia Cherahani kazi ambayo ameifanya mpaka alipofariki tarehe 16/01/mwaka 1999. Lakini pia aliweza kurudi darasani na kusoma elimu ya watu wazima katika Taasisi ya elimu ya watu wazima katika miaka ya 1970.
Salim Ali Kibao - 1953
Shauku ya kuanza kutunga na kuandika Mashairi, hadithi na tenzi ilimuanza katika miaka ya 1950, japokuwa kazi hii ya uandishi si ngeni katika familia ya kibao kwani babu yake mwenye jina hilo la Kibao, Sheikh Hemed bin Abdalla aliandika vitabu kama UTENZI WA ABDURAHMAN NA SUFIANI, VITA VYA WADACHI KUTAMALAKI MRIMA n.k pamoja na baba yake Sheikh Ali bin Hemed bin Abdalla Al-buhry alikuwa kadhi wa Tanga lakini pia alikuwa mshairi na mashairi yake yalikuwa yakipatikana katika gazeti laMambo leo katika miaka ya 1950.
Alianza kidogo kidogo kuandika mashairi akishindana na kaka zake kama Sheikh Mohammed Ali Al-buhry na wengineo hatimae alielekea Kenya na kuishi huko kwa zaidi ya miaka kumi na kusababisha kuingia katika mashindano ya  Jomo Kenyatta Prize for Literature mwishoni mwa miaka ya 1960, ndipo alipofanikiwa kuchukua nafasi ya kwanza Kwa kitabu chake cha UTENZI WA UHURU WA KENYA,maadhimisho yake yalikuwa mwaka 1973, ni kitabu cha pili katka mfululizo wa vitabu vya utenzi uitwao Vito vya Kiswahili kilichochapishwa na Oxford University Press.
Katika kitabu hicho Salim .A. kibao anasimulia jinsi waafrika wa Kenya walivyopigania uhuru wao chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta pamoja na viongozi wengine waliokamatwa, walivyohukumiwa na kufungwa na hatimae akaja kuiongoza nchi ya Kenya kwenye uhuru wake.
 
Kitabu hiki si cha historia ya Kenya lakini mwenye kukisoma hawezi kuepuka kuijua lau kwa muhtasari historia ya nchi ya Kenya, kwani mengi yaliyo muhimu kwenye historia ya Kenya, Salim .A.Kibao ameyadokeza – tena kwa lugha nyepesi.

Miongoni mwa mambo aliyoyadokeza ni Kesi ya Kenyatta na wenziwe; harakati za Mau Mau na jinsi mkoloni alivyoanzisha homgadi kuzipinga; juhudi zilizofanywa na vyama vya wilaya kuendeleza vita vya uhuru baada ya KAU kupigwa marufuku; kuundwa kwa KANU,KADU na APP na migogoro iliyotokea; uhuru kamili pamoja na kuvunjwa katiba ya majimbo; Oginga Odinga na KPU; na mzozo wa Shifta ni baadhi ya yaliyomo kwenye kitabu hicho.

Lakini pia mwaka 1975 alibahatika kuchapisha kitabu chake cha pili cha Hadithi kinachoitwa MATATU YA THAMANI, kilichochapishwa na Heinemann Educational Books.Kitabu hiki kinamhusu kijana mmoja aliyenunua maneno matatu ya thamani na hatimae kumweka katika utajiri mkubwa ilhali alikuwa masiki wa kutupwa.

Kwa Ufupi kabisa kitabu kinaelezea hadithi ya watoto watatu wa bwana Hogo ambao ni Hamu, Mazoea na Sudi, Mzee Hogo alipofariki dunia watoto wake waligawana mali. Hamu na Mazoea amabo ni wakubwa walichukua sehemu kubwa ya urithi na kumwachia mdogo wao Sudi sehemu ndogo sana. Wawili hao waliyavamia maisha ya anasa na baada ya muda si mrefu ufukara uliwafikia na kuweka makazi. Sudi alikwenda nchi ya mbali na kununua maneno matatu ya thamani – Ukitumwa tumika, Ukiaminiwa Jiaminishe na Ukiona la ajabu liangalie. Maneno hayo yalimfaa sana Sudi katika maisha yake; kwani alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo ya mbali. Ndugu zake ambao walimdhulumu na ambao maisha yalikuwa yamewaharibikia walikwenda kumwangukia miguuni na kumuomba msamaha.

Salim Ali Kibao akiwa na rafiki zake Kenya miaka ya 1970

Mwaka 1976, Salim .A. Kibao alifanikiwa kuwa mshindi wa pili kutoka kwa waandishi wanaotoka Tanzania katika uandishi wa mashairi aliyoshiriki huko Lagos Nigeria. ASILI YA MWAFRIKA ndio tenzi ambazo aliingia nazo katika mashindano hayo yaliyoshirikisha waandishi mbalimbali Afrika na lugha tofauti tofauti barani kwetu. kwa ufupi kabisa Asili ya mwafrika inaelezea namna waafrika walivyoishi kabla ya kutawaliwa na wakoloni, wakati wa ukoloni na namna tamaduni za waafrika zilivyoingiliwa na hatimae kupigania uhuru.
Mnamo mwaka 1988, Salim .A. Kibao aliandika kitabu kinachoitwa USHINDI WA MAISHA, chini ya UNESCO pamoja na Network of Education Innovation for Development in Africa (NEIDA) chini ya mradi wa Regional programme of publications in African Language, kitabu kilichochanganya Hadithi pamoja na mashairi.

Kitabu kinahusu maisha ya kijana Tega amba alikuwa ni kijana wa kipekee kabisa wa Mzee Kale ambae alifahamika katika kijiji cha Karibani kwa maarifa na busara zake. Lakini kijana huyo aliishi maisha yasiyoeleweka na kumletea matatizo mengi sana pamoja na mzee wake, uandishi wa mashairi unabeba ujumbe wa kuwaonya, kuwashauri na kuwanasihi vijana na maandishi ya kawaida yanaelezea maisha ya kila siku ya familia ya Mzee Kale na majirani zake.
 
Na pia aLIshinda katika kusheherekea MIAKA KUMI YA UHURU WA TANZANIA na mashIndano hayo yaliitwa kwa jina hilo na mashairi aliyotunga yaliitwa kwa jina hilo pia mnamo mwaka 1971.
Salim Ali Kibao - ofisi za UKUTA - 1995
Mbali na vitabu hivyo Salim Ali Kibao pia kuna miswada ya vitabu vingi amabavyo adi anafariki hakuweza kuvipiga chapa. Miongoni mwa vitabu hivyo ni SUBIRA, huu ni utenzi, LIANDIKWALO HALIFUTIKI, hii ni hadithi, KANZI YA LUGHA, FANI ZA USHAIRI, UTENZI WA ASILI YA MWAFRIKA na NAMNA YA KULITUNGA SHAIRI LA KISWAHILI NA KULIFUMBUA.
      
Salim Ali Kibao pia alikuwa ni mjumbe wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa vipindi vitatu mfululizo kwa kuchaguliwa na Waziri anaehusika na lugha ya kiswahili na ni pia alikuwa ni mwanachama na mwanakamati shupavu katika chama kinachoshughulikia kiswahili Tanzania – UKUTA (Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania.)

Toka mwaka 1972, Salim Ali Kibao alikuwa akishiriki katika vipindi mbalimbali vya lugha ya kiswahili vilivyokuwa vikifanyika katika Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990.



(Historia hii ni kwa hisani kubwa ya familia) 

No comments:

Post a Comment