HADITHI FUPI Na. 6
JINA: CHAUSIKU
MTUNZI: ISIHAKA ‘NUKTA’
KIBAO
Kwa kweli sikujua nifanye nini kwani nilikuwa na majonzi makubwa katika
maisha yangu, hakuna kilichoniendea sawa. Kila mtu nimtafutaye alikuwa ni kama
vile anaenisikiliza na kunipa ahadi nyingi za kunisaidia, wengine wakinambia
tutakupigia simu, wengine niwape muda mambo yao sio mazuri na wengine
kutokunipokelea simu kabisa.
Hali ya maisha kwangu ikawa ngumu
zaidi pale nilipokimbiwa na Chausiku ambaye nae nilitegemea nitakuwa nae kupika
na kupakua huko maisha yetu ya mbele. Nikaja kusikia tu kachumbiwa na mtu
mwenye pesa na kuolewa mji wa mbali. Ndipo nikakumbuka usia wa Baba,
aliponambia;
“Maisha yanapanda na kushuka,
ukiona maisha yanakuwia magumu sana rudi kwa Mungu, yeye nde mtatuzi wa kila
kitu.”
Haikuwa kazi ndogo kwani
nilikumbana na mtihani mkubwa ambao unaitwa ‘Subira’, ilikuwa inahitaji ujasiri
kusubiri maombi yangu kujibiwa na Mwenyezi kwani yeye ndie anajua muda gani
akujibu ambao utakuwa muafaka. Hivyo sikuacha kumuomba kila siku nikiamini
kwake kila kitu kinawezekana.
Ilipita miezi mitatu kwa hali ile ndipo siku moja
alfajiri nikatoka nyumbani mapema na kuamua kuzungukia maeneo ya sokoni
Kariakoo, palikuwa ni sehemu ambayo watu hawalali. Muda wote watu
wanashughulika, kwa alfajiri ile tayari soko lilikuwa lishajaa. Hata hivyo kwa kuwa pale ni katikati ya mji
na wengi huja mapema kuchukua mahitaji yao,
nilikatiza mitaa ile na ndipo
nikakumbana na ile hali ya kuthibitisha usemi wa “Milima haikutani ila binadamu
hukutana”.
Nikamuona Chausiku yuko kwenye gari nzuri akiwa anaongea na mwanaume,
sikutaka kumuita kwani kwa wakati ule sikuweza kufanya chochote. Hivyo nikabaki
namuangalia huku moyo ukiniuma kwani nilikuwa nampenda sana ila ndio hivyo kwa
kuwa nilikuwa sina uwezo, akanitelekeza.
Labda pia elimu yangu ndogo (Kidato
cha nne) hivyo nisingeweza kufanya kazi za ofisini, sikuwa na pesa ya kumtunza,
kumpa mtaji mkubwa wa biashara, kujenga nyumba na kuwa na gari… basi alimuradi
mawazo yakawa mengi kichwani mwangu.
Ila baada ya muda yule bwana
akashuka na kuingia ndani ya moja ya maduka pale karibu, moyo ukapata ujasiri
kama vile mtu alieambiwa wakati ni huu, kufa au kupona. Nikajikaza na kuinua
hatua moja moja mpaka nikafika pale alipo na kugonga kioo cha gari. Alishtuka
sana Chausiku na kuniangalia mara mbili mbili. Nikamuita
“Chau… Chausiku, ni wewe?”
Akainamisha macho chini na kutaka
kujifanya hajasikia. Nikamgongea tena kioo kwa kumuita
tena, alipoona sikati tama na yeye hakutaka liwe kubwa jambo akashusha kioo cha gari na kuona haya maana
tokea ameolewa ilikuwa imepita miezi minne na hakunambia chochote. Alipomaliza
kushusha kioo kumuangalia vizuri nikaona kitu cha kunishtua, alikuwa amebadilika, tumbo limeongezeka.
Nikamuuliza “Chau wangu una uja
uzito?”
Akaanza kubabaika “Ahh ah.. Mashaka,
mbona uko mitaa hii?”
Nikamuuliza tena “Chau wangu,
nilikukosea nini? Si ungenambia kama hunipendi kuliko kunisaliti namna hii?
Moyo wangu uliacha kwenye wakati mgumu sana. Siku nasikia tetesi unataka
kuolewa moyo nilihisi kama unataka kusimama kwani sikudhania kama ni Chau wewe.
Na mwenzangu hukunambia chochote, kumbe ilikuwa unanipaka mafuta kwa mgongo wa
chupa. Ni bora ungenambia ukweli tokea mwanzo kama kwangu ulikuja kunipotezea
muda, angalia umenifanya nipoteze mwelekeo ndani ya muda mfupi. Kazi yangu ya
kusambaza maji nilikuwa nakuaibisha sana kumbe, nilikuwa nachomeka na jua kwa
sababu nilikuwa najua tuko wawili, kumbe mwenzangu ulikuwa haupo kwenye msafara
wangu. Ulikuwa abiria wa ndege uliepanda mkokoteni, nakushkuru kwa funzo
ulonipa."
Wakati nataka kuendelea kumtolea
ya moyoni nikamuona yule bwana anajitayarisha kutoka mule dukani. Nikamuangalia
kisha nikatabasamu, nikamwambia Chausiku;
“Inaonekana ulikuwa unanisaliti
muda mrefu, haiwezekani ujauzito huo… daaah… nashkuru sana… mungu atanilipia,
kwa heri”
Niliamua kuondoka maeneo yale
kwani siku yangu tayari ilikuwa ishapoteza dira, hata mipango yangu ya kutafuta
hela nikaona sielewi sielewi. Nikaamua kunyoosha zangu njia niliyotokea na
kurudi nyumbani kigogo, huku nyuma yule bwana aliingia kwenye gari na kuondoka
na Chausiku. Baada ya dakika kumi na tano hivi nikasikia makelele yanatokea kama mtaa wa
pili kutoka pale nilipo na watu wanendea huko kwa kasi kana kwamba kuna tukio.
Nikaona nami niende nikashuhudie, kufika pale nikaona watu wamejaa wengi na kuzungukia
eneo lile. Nikaamua kusogea karibu zaidi,
nikagundua ni ajali imetokea pale.
“Pikipiki na gari zimegongana”
“Huyu wa pikipiki alikuwa anakuja
kwa kasi,
hakuangalia vizuri kamvaa mwenye gari”
“Hawa boda boda bwana, kila siku
wanakufa”
Zilikuwa kauli ambazo zinatoka
eneo lile, likiashiria ajali ya pikipiki na gari. Nikajipenyeza mpaka nikafika
karibu zaidi na kugundua ni gari alimo Chausiku na yule jamaa. Roho ikanipasuka na kuanza
kuita;
“Chausikuuuuu, chausiku! Chau…”
Watu pale wakanishangaa na
kunipisha, huku wanione nitafanyaje?
Wengine wakawa wananiuliza, “Vipi
unawafahamu hawa?”
Nikajibu “Ndio, nawafahamu hawa,
huyu mwanamke ni Chausiku. Nimetoka kuwaacha hapo nyuma muda sio mrefu”
Wakati nikisema yale kwa bahati,
Askari wa Barabarani akawa kashafika kwa kushughulikia ajali ile. Wakatokea
wasamaria na kuchukua majeruhi wale, yule mwanaume akiwa kaumia vibaya kwani
upande wake ndio pikipiki ile iligonga. Wakati wanachukuliwa majeruhi namimi
nikachukuliwa kwani ndie niliekuwa nawafahamu.
Safari ilitoka pale mpaka
Muhimbili kitengo cha dharura huku njiani nikiwa namuomba Mungu lisitokee
lolote kwani nitazidi kuchanganyikiwa ikiwa Chausiku hatoamka.
Kila nikimtazama fahamu yake
haiku vizuri, ananung’unika tu maumivu huku akishika tumbo lake. Yule bwana ndio
alikuwa katulia tu kwani alipoteza fahamu kwa muda.
Tulifika hospitali na
wakaingizwa kwenye kitengo maalumu nami nikawaandikisha nikiwa kama rafiki yao.
Sikuwa na simu ya kuwajulisha wazazi kwani hata hivyo namba zao nilikuwa
sizifahamu, niliweza kuazima simu na kumpigia rafiki yake Chausiku aitwae
Sabrina. Huyu namba yake niliweza kuihifadhi kwenye kijitabu changu kidogo na
kumpa habari ya ajali, alipata mshituko kwani hakuweza kujizuia na kunambia
atakuja muda sio mrefu.
Baada ya masaa mawili kutokana na
umbali anakoishi Sabrina aliweza kufika pale na kunikuta hospitali nikiwa
nimenyongea. Kwa bahati wale wasamaria waliweza kutuacha na tukawashukuru kwa
msaada wao mkubwa walioufanya.
“Haya vipi shemeji, ilikuwaje?”
Sabrina ananiuliza
Nami nikamueleza habari yote ya
ajali huku macho yangu yakiwa yakiwa yana uwekundu kwa mbali nikijikaza
kutokana na kulia. Ile hali ya macho yangu haikuweza kujificha kwani hata
Sabrina aliiona na kunipoza pamoja na kunipa moyo.
Nikamgeukia, na kumwambia “Sabrina,
Chausiku nilitokea kumpenda sana na mpaka nasikia tetesi za kutaka kuolewa
niliumia zaidi na kibaya kingine alinificha.”
Baada ya kuongea hayo nikaona
Sabrina kama vile kapoa na kutazama pembeni. Sikujua kwa nini, nikaendelea,
“Leo kama Mungu namuona mitaa ya
Kariakoo, namuuliza lakini bado hakuning’azia, halafu ni mja mzito Sabrina. Hii
ina maana alikuwa ananisaliti kipindi tuko wote? Hivi wewe ulikuwa unafahamu
yote haya? Mbona hukunambia mchezo wote huu mpaka mimi nafanyiwa haya,
hukunitakia mema kwa rafiki yako?”
“Sikiliza shemeji” aliongea Sabrina
“Mimi ndie rafiki yake mkubwa
Chau, na kwa sasa embu tufanye kumuombea mungu kwanza jambo hili lipite. Hayo
mengine yataongeleka huko mbele, … lakini…”
Wakati anaendelea, Daktari
akatokea na kuita
“Mwenye Mgonjwa wa Chausiku”
Nikasimama haraka na kumfuata
Daktari, “Ni mimi hapa”
Daktari akanishika begani na
kunambia “Nina habari nataka kukupa, tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu na
tumepambana sana”
Daktari alinitia hofu na
kunifanya nisimame vizuri kumskiliza kwa makini
“Majeruhi wetu wa kume hatunae
tena, ametutoka. Ni kazi ya mungu kwani amevujia damu ndani kwa ndani,
hatukuweza kufanya zaidi ya kile tulichojaaliwa. Ila Chausiku anaendelea vizuri
kwani fahamu zimerudi vizuri na baadae kidogo mnaweza kwenda kumuona.
Tumegundua pia alikuwa mja mzito ila uja uzito wake kwa uchunguzi wa awali
unaonekana hauja athirika ila tutaendelea kumchunguza zaidi tena kujiridhisha”
Baada ya kuongea maneno yale
Daktari yule aliniacha na kuendelea na majukumu yake mengine. Nilishusha pumzi
nzito kama mtu aliyekuwa amebeba dunia mabegani mwake, nikamfuata Sabrina na kumpa
habari zile. Sote tulishukuru mungu kwa Chausiku kuwa na afya njema na kupona
mtihani ule, hivyo tukaenda nje kwa ajili ya kumuacha Chausiku aendelee
kupumzika huku tukifanya jitihada za kuwapigia simu wazazi wake kwani mwenzangu
Sabrina alikuwa na simu.
Tulielekea kwenye mgahawa pale
pale Muhimbili ndani kwa ajili ya kupumzika huku tukisubiria Chausiku apate
mapumziko kutokana na hali yake, hatimaye tukawapata wazazi wa Chausiku na
kuwapa habari ile. Iliwashtua sana ila kwa kuwa walikuwa wanamfahamu Sabrina vizuri
walimwambia amsimamie mpaka wao watakapofika, kwani wao walikuwa wanatokea
Kibaha.
Baada ya Sabrina kuwataarifu
wazazi wa Chausiku kuhusu ajali ile. Nikamgeukia na kumuuliza, “Ulikwa unataka
kusema kitu kabla Daktari hajaja?”
Sabrina aliinama chini na kuanza
kunielezea.
“Najua mimi sio muhusika na
msemaji wa maneno haya, ila ukweli ni kwamba, Chausiku anakupenda sana wewe.
Ile ndoa alilazimishwa na Baba yake kwani walikuwa hawakutaki wewe sababu ya
elimu na pesa, waliona mtoto wao anateseka na wao hawafaidiki na chochote.
Hivyo wakaamua kumlazimisha kuolewa na yule bwana, yule bwana anaitwa Karim ni
wale wasomi waliosoma nje ya nchi, aliagiza atafutiwe mchumba na mzee ndio
akalazimisha.
Chausiku hakujua hilo, ila Mzee
wake alitumia ujanja wa kumuita kijijini na kumlazimisha ndoa, ndio maana
kipindi kile alivyokuaga anaenda nyumbani akachelewa kurudi, ikawa hapatikani
hewani kwani simu alipokonywa. Hata mimi alikuja kunipigia simu baada ya wiki
tatu na kunambia ukweli ila nikashindwa kukutafuta kwani wewe nawe huna simu na
pale Tandika ulipokuwa unakaa ukahama. Hivyo ikawa ngumu kukupata lakini sio
kweli kama alikuwa anakusaliti na hilo swala la mimba hakuniambia chochote”
Tulikaa mpaka mida ya alasiri
kwani hakuna kati yetu aliyeweza kuinua miguu yake na kuelekea kwenye shughuli
nyingine, Sabrina alinieleza kinaga ubaga ni kwa kiasi gani Chausiku alikuwa
hakubaliani na ile ndoa ila kwangu ilikuwa ni kama usiku wa giza kwa kipindi chote
hicho. Nikajisemea moyoni
“Ndio maana hakuweza kunijibu chochote kwa kipindi
kile namuhoji kwenye gari – nilikuwa namshutumu bure”.
Nikajiapiza kumsikiliza
na kutomshambulia tena pindi atakapokuwa yuko salama. Baada ya muda kidogo, nikamshauri
Sabrina twende ndani tukamuangalie Chausiku kwani ni masaa kadhaa yamepita na
twaweza ruhusiwa kumuona japo kwa uchache. Tuliingia ndani na kwenda moja kwa
moja maulizo kwa wauguzi na kuuliza.
Tukaelekezwa wodi alipopelekwa, tukaenda
kumuona, ijapokuwa hakuwa na nguvu za kuongea sana ila aliponiona tu machozi
yalimtiririka mashavuni mwake na kulia kwa uchungu.
Nikamuwahi kwa kumshika mkono na
kumwambia, “Sabrina ameshanieleza yaliyokutokea kipindi chote hichi. Nisamehe
mimi kwa kukushutumu ila sikuwa najua”
Chausiku alitabasamu kwa mbali
ila hakuweza kunijibu chochote na akaishia kuangalia tumbo lake akiwa na
wasiwasi na kiumbe kile alichobeba. Nikamsogelea kwa karibu zaidi na kumueleza,
“Daktari ametuambia uja uzito uko
salama, umepata mshtuko kidogo ila wataendelea na uchunguzi zaidi hapo baadae”.
Maneno yangu yalimtia nguvu kama
vile mtu aliekata kiu baada ya kukaa nacho kwa mrefu. Aliuinua mkono wangu na
kuupeleka kwenye tumbo lake kisha na kuniita
“Mashaka”
“Huu ujauzito ni wako, ilikuwa
siri yangu. Kabla sijakwambia ndipo nikapigiwa simu na baba ananiita nyumbani,
nikasema nikirudi nije nikushtukize ila haikuwa hivyo. Nina mengi ya kukueleza
ila nilipitia mengi kwa yule bwana kwani hakuwa mume mwenye mapenzi na huruma
kwangu. Alinidharau kwa kuwa ni maskini na sikusoma, niliomba Mungu kila siku
anitoe kwenye mtihani ule, na sikuweza kumwambia kuhusu mimba hii kuwa sio ya
kwake, alijua ni yake kwani angezidi kuninyanyasa. Siamini kama ndio wewe ulienisaidia mpaka
nimefika hapa”
Nikautoa mkono wangu tumboni
mwake na kumfuta machozi usoni mwake na kumwambia;
“Chausiku, siamini unachoniambia.
Moyo wangu umepata mshtuko ghafla, huu uja uzito uliondoka nao kipindi kile? Ama kweli Mungu ni mkubwa, leo amenikutanisha na mwanangu. Nitakutunza Chau
wangu, nitaendelea kupambana kwa kadri niwezavyo mpaka mtoto azaliwe na uwe na
afya nzuri”
Baada ya kunambia maneno yale, tukamtaarifu habari ya msiba wa yule mwanaume aliyekuwa nae.
Cha ajabu Chausiku hakusikitika wala kujuta, aliishia tu kuitikia na kusema;
"Hakuna amuombeaye mwenzio kifo ila ni ahadi yake ilikuwa imefika, Mashaka - yule ndio alikuwa Karim, mume wangu nilieishi nae kwa mateso. Haikuwa kazi rahisi na ujauzito huu, ni mungu tu ndiye aliyekuwa ananisitiri, nisingependa tuendelee kuongea sana kuhusu yeye.
Nimefurahi kukuona Mashaka, amani imerudi moyoni mwangu. Ila nahisi kuishiwa nguvu, natamani niendelee kuongea nawe"
Baada ya kusema vile tukaona mimi na Sabrina tumuache apumzike kwa uchovu alokuwa nao.
^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^
Tulikuwa tunatoka kliniki na Mama
Harith huku mtoto akiwa amelala kwa kuchoka kwani tulienda kupima uzito tu na
kuondoka. Chausiku alikuwa ni mama mwenye afya maridadi huku nami nikiwa
nimeota kitambi kwa mbaali cha kufutia simu ya ‘touch’ – smartphone. Maisha
yetu yalikuwa mazuri kwani hatimaye niliweza kumuoa Bi Chau baada ya kuwa mjane
na kisheria kurithi mali za marehemu mumewe, hivyo kupitia mali zile tuliweza
kufanya mapinduzi ya kimaisha baada ya kunisihi sana tuzitumie kujenga penzi
letu na maisha yetu.
Kwa kuwa tulipendana sana, hali
ile tukakubaliana nayo nami nikakubali kuanza maisha naye kwa uwezo ule wa
kifedha alokuwa nao. Tuliweza kwenda kijijini kwa wazazi na Chausiku aliweza
kutoa msimamo wake juu yangu na kutaka nimuoe kwani mie die mwanaume anitakae
kimaisha na anipendae ikiwa ni pamoja na kuwa ni mzazi mwenzie. Wazazi safari
hii hawakuwa na pingamizi kwani walijua kilichomtokea mtoto wao na hivyo
kututaka radhi na kutuambia kwamba
“Shetani na tama zilituponza
wanetu, hivyo kwa sasa sisi hatuna pingamizi. Tuko radhi na ndoa na mnaweza
kuoana”
Hivyo jambo la ndoa likapita, tukapata
mtaji mzuri wa kuanzisha biashara ya usambazaji maji kupitia ofisi kubwa ya
uwakala tulioanzisha na pia tuliweza
kujimudu kujenga nyumba kwa ajili ya wazazi wa Chausiku na mara kwa mara ilikuwa tukiwatembelea na
kuwapelekea mjukuu wa kucheza nao na hivyo hawakuwa na namna ya kukubali na
kubariki maisha yetu
MWISHO
No comments:
Post a Comment