Ni mimi muandishi na msimamizi wako wa Blogu hii Isihaka S. Kibao; Ni mhitimu wa Shahada ya kwanza ya Usimamizi wa Ugavi na Manunuzi kutoka chuo cha Kilimo cha Sokoine (Sokoine University of Agriculture - SUA). Nilipata shahada yangu hii ya kwanza mwaka 2013 na kuweza kujiendeleza katika elimu mbali mbali za ujasiriamali na kujifunza zaidi uandishi wa mchanganuo wa biashara katika Chuo cha SUA na uandishi wa Maombi ya Miradi katika Jiji la Dar es Salaam kupitia kozi mbali mbali.
Mbali na hayo yote, akili yangu na uwezo wangu kiuandishi haukucheza mbali nami kwani kilichopo katika uwezo wako damuni hubakia pale pale na ulimwengu hufanya kukunoa dhidi ya hiko mpaka pale utakapoamua kukitumia kulingana na ukali wake. Safari yangu ya uandishi imeanza kutoka mbali, nikimaanisha tangu mzee wangu Mzee Salim Ali Kibao aliekuwa mwanaharakati wa mbinu za lugha ya Kiswahili fasaha na aliekuwa akipigania matumizi ya Kiswahili katika nchi yetu ya Tanzania na Afrika Mashariki alipofariki mnamo mwaka 1999 (Historia yake inatambuliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania BAKITA), historia yake itakujia baadae kidogo. Ijapokuwa kipindi hicho nilikuwa mdogo na si mpevu sana kiakili.
Nilivutiwa na uandishi wake wa hadithi na mashairi kwani aliweza kutunga vitabu vingi na hadithi nyingi mpaka nyingine kumpatia tuzo za uandishi nchini Kenya (Historia itaelezwa mbele). Sikuona ajabu yeye kufikia huko kwani alikuwa anaweza.
Hivyo nami bila kujijua nikaanza kuandika kidogo kidogo, kuanzia mashairi mpaka hadithi fupi fupi na ndefu. Kuogelea kwenye bahari ya uandshi sio kazi ndogo kwani yataka utashi, mavumilivu na ushirikiano kutoka kwa wadau wengine. Hivyo baada ya kukaa kwa muda mrefu nje ya duru hili la uandishi kwa muda mrefu nami nimeamua kurudi tena nikiwatayarishia wasomaji wangu mambo yatakayo wavutia na kuwatia hamasa na ikibidi kuwafunza kupitia NUKTA zangu nitakazokuwa naweka.
NUKTA ni alama inayotumika katika sentensi, neno au kifungu cha maneno na matumizi yake hasa ni kuonesha ukomo wa sentensi, neno au kifungu cha maneno. Hivyo NUKTA yangu ni kuonesha kwa jinsi gani MANENO yangu au HADITHI zangu zitakuwa mwisho wa taharuki, hamu, fikra au hali yoyote itakayokuwa katika fikra zako dhidi ya upande mwingine wa uelewa.
Ntumia nitashawishi na kuvutia kufikia malengo ya NUKTA kwako msomaji wangu.
Ni mimi Isihaka SK
#Nukta
No comments:
Post a Comment