JINA - "SALMA"
MTUNZI : ISIHAKA 'NUKTA' KIBAO
Yalikuwa matone
ya damu yakinimwagika kwenye mkono wangu mithili ya bomba la maji ambalo
halijafungwa mpaka mwisho, sikuweza kuinuka kwani sikuweza kabisa kuinua miguu
yangu. Kila nikiitazama na kujitahidi kuiinua naona kana kwamba miguu ile si
yangu. Sikuweza kufanya chochote. Kwa mbali nikasikia watu wakipiga yowe huku
wakielekea upande nilipo.
“Ajaliiiiii…
njoooni huku, pia kuna watu”
Sauti ile,
yasemekana ilikuwa ya ukali na ya nguvu lakini kwa upande wangu ilikuwa ni sauti
yenye kufifia na kutoskika vizuri. Sikuweza hata kumjibu mwana mama yule ambaye
alikuwa na nia ya kunisaidia eneo lile. Nikashkuru kwa kelele zake kwani
niliishia kuona kundi la watu likinizunguka kwa idadi kuongezeka huku mie macho
yangu yakiishiwa nguvu na kufumba. Nikapoteza fahamu.
Baada ya muda
nafumbua macho na kuangaza kila pembe pale mahala nilipo nikagundua nimelala
kwenye kitanda chenye maandishi makubwa “MSD”. Nikajiuliza katika akili yangu
na kugundua niko hospitali kwani harufu za dawa na wagonjwa wengine kwenye
vitanda vingine nao pia walikuwa wakinitazama. Wengine kwa mshangao, wengine
kwa kutokujali na wengine waliendelea na shughuli zao.
Kitanda cha
pembeni yangu nilichokuwa nimelala alikuwa amelala kijana mmoja, rika langu,
nikamtazama na kumuangalia vizuri nikaona amekatwa mguu mmoja. Nikajiangalia na
mie nikaona miguu bado ninayo ila siwezi kuisogeza, nikamuita na kuanza kuongea
nae.
“Habari yako”
Akanijibu “safi”
Nikamuuliza
“hapa ni wapi?”
Akanijibu “Hapa
ni Tumaini Hospital”
Akanitazama kwa
dakika kadhaa na kuniambia
“Unajua sisi
binadamu tunajidai sana na kujisahau hali ya kuwa kabla hatujafa hatujaumbika,
kwa maana ulivyoletwa juzi ulikuwa huna fahamu kabisa. Tukajua wewe ni
safari, hutaamka. Ila ushUkuru sana, Mungu kakurudisha tena, unapaswa kumrudia
kwa nguvu zako zote rafiki yangu”
Alivyonambia
vile, nikajiinamia na kuvuta kumbukumbu mara ya mwisho nilikuwa wapi. Mbali na
kile alichonambia, akili yangu ikawa inawaza miguu yangu tu, kwa nini siwezi
kuinuka. Baada ya muda kidogo nikamuona Salma anakuja na daktari huku wakiwa na
kiti cha magurudumu “Wheelchair”. Nikashtuka sana nikajisemea,
“Mungu wangu
ndio nimeshakuwa kiwete? Itakuwaje? Maisha yangu yatakuwaje? Malengo yangu je?"
Yakanijia
maswali mengi sana kichwani mwangu ila kabla sijaendelea na mawazo yale, Salma
na Daktari wakawa wameshafika pale kitandani kwangu.
Salma alikuwa ni
msichana mwenye upendo wa kweli sana, alinipenda bila ya kujali tabia yangu ya
ujana kwa kupenda starehe za pombe, muziki na ulevi wangu mwingine mkubwa wa
mapiki piki. Alikuwa kila siku akinisihi niache tuyajenge maisha ila sikuwa
nampatiliza. Salma kwao walikuwa ni watu wenye uwezo sana wa kifedha kwani baba
yake alikuwa Balozi mstaafu. Hivyo pesa haikuwa ikiwapiga chenga.
Alinifuata
karibu yangu na kunisalimu,
“Habari Zaki,
Umeamkaje leo?”
Nikamuitikia
Salamu kiunyonge na kumwambia “Nashkuru nimeamka salama. Nina uchovu mwingi tu”
Salma
aliniangalia usoni kisha akaitazama miguu yangu, alijua nilichokuwa nakitarajia kutoka kwake
kuhusu maelezo ya Daktari maana uso wangu ulikuwa na maswali yote ambayo
yalijionesha bila ya kutamkwa na kinywa.
Salma aliendelea kuongea, “Zaki,nilipigiwa
simu na Melanie, alikuwa karibu na tukio la ajali uliyopata na
kunieleza kilichotokea na wapi ulipelekwa. Usijali, kwani nilikuwa
nikikusimamia tokea juzi, na sikukata tamaa kwani nilijua utaamka ijapokuwa nilijawa na hofu juu ya hali yako. Nilimuomba
sana mungu usiku kucha na namshkuru kwani dua zangu alizijibu”
Nikamtazama usoni na nikamuita
“Salma, nashkuru sana kwa yote ulionifanyia, sina la kukulipa. Ila miguu yangu, siwezi kuisogeza.”
Nikamgeukia
Daktari, “Dokta, miguu yangu vipi? Nitafanyaje kazi zangu, maisha yangu
yatakuwaje?”
Daktari alisogea
karibu na kunishika bega, kisha kunambia
“Zaki, pole
sana. Ulipata ajali mbaya ya pikipiki na tunashkuru umeweza kupambana
umerudi leo uko nasi tena, tumefanya uchunguzi wa awali kuhusu miguu yako. Kwa
bahati daktari wetu bingwa alikuwepo jana usiku, anaehusiana na mishipa. Kwa mujibu wake
anasema utakuja kutembea na kuendelea na shuguli zako kama kawaida. Ajali
uliyopata imesababisha baadhi ya mishipa yako ya fahamu kuminywa na kupeleka
mawasiliano hafifu kuendea hakuna kutokea kwenye uti wa mgongo kuelekea miguuni
kwa sababu pingili za uti wa mgongo zimeshtuka na kusababisha hayo.
Unapaswa kutumia
dawa na mazoezi ya viungo ili urudi kwenye hali yako ya kawaida. Itakuchukua
muda ila utapona, ni juhudi tu, bila ya kukata tamaa.”
Kwa maneno yale,
nikajisikia vibaya kwani ajali ile ilikuwa ni sababu ya mwendo kasi wangu.
Hivyo nilijitakia mwenyewe, lakini maelezo yale ni kama yalikuwa kinyume kwa
Salma kwani alitabasamu na kunishika mkono na kunambia.
“Zaki, daktari
ametuthibitishia kuwa utatembea. Kwa hivyo kwa sasa ni dawa na mapumziko ya
kutosha”
^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^
Baada ya mwaka
kupita sikuamini kama ningeweza kukunja goti mbele ya Baba Mkwe mtarajiwa huku
Sheikh pembeni akitushikisha mikono na kututamkisha maneno ya kufunga ndoa baina ya
mimi na Salma. Salma alinitoa mbali, nilikuwa nikimdharau, kutokumjali na
kuutesa moyo wake. Ila alipigana na hali yangu mpaka nikaweza kutembea tena,
alikuwa akija nyumbani kila tarehe ya mazoezi ilipokuwa ikifika na kunichukua
kunipeleka hospitali na kunirudisha.
Moyo wake wa
ajabu ulinitia nguvu na nikatia nia kurejea kwenye hali yangu ya kawaida.
Ilikuwa kila nikimtazama sioni cha kumlipa zaidi ya nami kumzawadia moyo wangu
ambao alikuwa akiulilia miaka nenda miaka rudi. Salma kwangu-kwake nilikuwa
kama vile penye miti hakuna wajenzi, ila nilikuja nikalitambua hilo na
kumkubali ikiwa pamoja na kumpa moyo wangu. Hivyo baada ya ndoa tuliweza kujenga familia na tukaishi vizuri pamoja na kupata mmoja.
MWISHO
No comments:
Post a Comment