Thursday, 19 April 2018

April 19, 2018

MSEMO WA LEO: 19-04-2018


 
Theodore "Dr. Seuss" Giesel
Mambo yanapotokea huwa na matokeo mawili, furaha au huzuni itategemea unachukulia vipi hali utakayokutana nayo. Ila ni vizuri kuwa  upande chanya kwani jambo likitokea limetokea. Jifunze kitu kutoka kwa muasisi wa "Dr. Seuss" - MSEMO WA LEO

"Don't cry because it's over, smile because it happened." -- Dr. Seuss

"Usilie kwa kuwa yameisha, tabasamu kwa kuwa yamefanyika" -- Dr. Seuss


Kwa historia ya msemaji wa leo Ingia hapa:
April 19, 2018

MAGAZETINI LEO 19-04-2018

Wednesday, 18 April 2018

April 18, 2018

Msemo wa Leo: 18-04-2018


Mary Tyler

Uwerevu ni kitu kinachoanzia mbali sana, watu hupitia mengi na hatua nyingi. Yapo mahitaji ya kuwerevuka ili uwe hivyo. MARY TYLER anatufunza vitu vichache ili tuwe hivyo 
- MSEMO WA LEO

"Take chances, make mistakes. That's how you grow. Pain nourishes your courage. You have to fail in order to practice being brave."
-- Mary Tyler

"Tumia fursa, ingia makosani. Hivyo ndivyo utaendelea. Maumivu yanakuza ujasiri. Yakubidi kushindwa ili uwe na uwezo wa kutenda uwerevu."
-- Mary Tyler

  Kwa historia ya msemaji wa leo ingia hapa:
April 18, 2018

MAGAZETINI LEO: 18-04-2018

Saturday, 14 April 2018

April 14, 2018

HADITHI FUPI Na. 6 - CHAUSIKU


HADITHI FUPI Na. 6
JINA: CHAUSIKU
MTUNZI: ISIHAKA ‘NUKTA’ KIBAO
Kwa kweli sikujua nifanye nini kwani nilikuwa na majonzi makubwa katika maisha yangu, hakuna kilichoniendea sawa. Kila mtu nimtafutaye alikuwa ni kama vile anaenisikiliza na kunipa ahadi nyingi za kunisaidia, wengine wakinambia tutakupigia simu, wengine niwape muda mambo yao sio mazuri na wengine kutokunipokelea simu kabisa.

Hali ya maisha kwangu ikawa ngumu zaidi pale nilipokimbiwa na Chausiku ambaye nae nilitegemea nitakuwa nae kupika na kupakua huko maisha yetu ya mbele. Nikaja kusikia tu kachumbiwa na mtu mwenye pesa na kuolewa mji wa mbali. Ndipo nikakumbuka usia wa Baba, aliponambia;

“Maisha yanapanda na kushuka, ukiona maisha yanakuwia magumu sana rudi kwa Mungu, yeye nde mtatuzi wa kila kitu.”

Haikuwa kazi ndogo kwani nilikumbana na mtihani mkubwa ambao unaitwa ‘Subira’, ilikuwa inahitaji ujasiri kusubiri maombi yangu kujibiwa na Mwenyezi kwani yeye ndie anajua muda gani akujibu ambao utakuwa muafaka. Hivyo sikuacha kumuomba kila siku nikiamini kwake kila kitu kinawezekana. 

Ilipita miezi mitatu kwa hali ile ndipo siku moja alfajiri nikatoka nyumbani mapema na kuamua kuzungukia maeneo ya sokoni Kariakoo, palikuwa ni sehemu ambayo watu hawalali. Muda wote watu wanashughulika, kwa alfajiri ile tayari soko lilikuwa lishajaa. Hata hivyo kwa kuwa pale ni katikati ya mji na wengi huja mapema kuchukua mahitaji yao,
nilikatiza mitaa ile na ndipo nikakumbana na ile hali ya kuthibitisha usemi wa “Milima haikutani ila binadamu hukutana”. 

Nikamuona Chausiku yuko kwenye gari nzuri akiwa anaongea na mwanaume, sikutaka kumuita kwani kwa wakati ule sikuweza kufanya chochote. Hivyo nikabaki namuangalia huku moyo ukiniuma kwani nilikuwa nampenda sana ila ndio hivyo kwa kuwa nilikuwa sina uwezo, akanitelekeza. 

Labda pia elimu yangu ndogo (Kidato cha nne) hivyo nisingeweza kufanya kazi za ofisini, sikuwa na pesa ya kumtunza, kumpa mtaji mkubwa wa biashara, kujenga nyumba na kuwa na gari… basi alimuradi mawazo yakawa mengi kichwani mwangu.

Ila baada ya muda yule bwana akashuka na kuingia ndani ya moja ya maduka pale karibu, moyo ukapata ujasiri kama vile mtu alieambiwa wakati ni huu, kufa au kupona. Nikajikaza na kuinua hatua moja moja mpaka nikafika pale alipo na kugonga kioo cha gari. Alishtuka sana Chausiku na kuniangalia mara mbili mbili. Nikamuita

“Chau… Chausiku, ni wewe?”

Akainamisha macho chini na kutaka kujifanya hajasikia. Nikamgongea tena kioo kwa kumuita tena, alipoona sikati tama na yeye hakutaka liwe kubwa jambo  akashusha kioo cha gari na kuona haya maana tokea ameolewa ilikuwa imepita miezi minne na hakunambia chochote. Alipomaliza kushusha kioo kumuangalia vizuri nikaona kitu cha kunishtua, alikuwa amebadilika, tumbo limeongezeka.

Nikamuuliza “Chau wangu una uja uzito?”

Akaanza kubabaika “Ahh ah.. Mashaka, mbona uko mitaa hii?”

Nikamuuliza tena “Chau wangu, nilikukosea nini? Si ungenambia kama hunipendi kuliko kunisaliti namna hii? Moyo wangu uliacha kwenye wakati mgumu sana. Siku nasikia tetesi unataka kuolewa moyo nilihisi kama unataka kusimama kwani sikudhania kama ni Chau wewe. Na mwenzangu hukunambia chochote, kumbe ilikuwa unanipaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Ni bora ungenambia ukweli tokea mwanzo kama kwangu ulikuja kunipotezea muda, angalia umenifanya nipoteze mwelekeo ndani ya muda mfupi. Kazi yangu ya kusambaza maji nilikuwa nakuaibisha sana kumbe, nilikuwa nachomeka na jua kwa sababu nilikuwa najua tuko wawili, kumbe mwenzangu ulikuwa haupo kwenye msafara wangu. Ulikuwa abiria wa ndege uliepanda mkokoteni, nakushkuru kwa funzo ulonipa."

Wakati nataka kuendelea kumtolea ya moyoni nikamuona yule bwana anajitayarisha kutoka mule dukani. Nikamuangalia kisha nikatabasamu, nikamwambia Chausiku;

“Inaonekana ulikuwa unanisaliti muda mrefu, haiwezekani ujauzito huo… daaah… nashkuru sana… mungu atanilipia, kwa heri”

Niliamua kuondoka maeneo yale kwani siku yangu tayari ilikuwa ishapoteza dira, hata mipango yangu ya kutafuta hela nikaona sielewi sielewi. Nikaamua kunyoosha zangu njia niliyotokea na kurudi nyumbani kigogo, huku nyuma yule bwana aliingia kwenye gari na kuondoka na Chausiku. Baada ya dakika kumi na tano hivi nikasikia makelele yanatokea kama mtaa wa pili kutoka pale nilipo na watu wanendea huko kwa kasi kana kwamba kuna tukio. 

Nikaona nami niende nikashuhudie, kufika pale nikaona watu wamejaa wengi na kuzungukia eneo lile. Nikaamua kusogea karibu zaidi, nikagundua ni ajali imetokea pale.

“Pikipiki na gari zimegongana”

“Huyu wa pikipiki alikuwa anakuja kwa kasi, 
hakuangalia vizuri kamvaa mwenye gari”

“Hawa boda boda bwana, kila siku wanakufa”

Zilikuwa kauli ambazo zinatoka eneo lile, likiashiria ajali ya pikipiki na gari. Nikajipenyeza mpaka nikafika karibu zaidi na kugundua ni gari alimo Chausiku na yule jamaa. Roho ikanipasuka na kuanza kuita;

“Chausikuuuuu, chausiku! Chau…”

Watu pale wakanishangaa na kunipisha, huku wanione nitafanyaje?

Wengine wakawa wananiuliza, “Vipi unawafahamu hawa?”

Nikajibu “Ndio, nawafahamu hawa, huyu mwanamke ni Chausiku. Nimetoka kuwaacha hapo nyuma muda sio mrefu”

Wakati nikisema yale kwa bahati, Askari wa Barabarani akawa kashafika kwa kushughulikia ajali ile. Wakatokea wasamaria na kuchukua majeruhi wale, yule mwanaume akiwa kaumia vibaya kwani upande wake ndio pikipiki ile iligonga. Wakati wanachukuliwa majeruhi namimi nikachukuliwa kwani ndie niliekuwa nawafahamu. 

Safari ilitoka pale mpaka Muhimbili kitengo cha dharura huku njiani nikiwa namuomba Mungu lisitokee lolote kwani nitazidi kuchanganyikiwa ikiwa Chausiku hatoamka.
Kila nikimtazama fahamu yake haiku vizuri, ananung’unika tu maumivu huku akishika tumbo lake. Yule bwana ndio alikuwa katulia tu kwani alipoteza fahamu kwa muda. 

Tulifika hospitali na wakaingizwa kwenye kitengo maalumu nami nikawaandikisha nikiwa kama rafiki yao. Sikuwa na simu ya kuwajulisha wazazi kwani hata hivyo namba zao nilikuwa sizifahamu, niliweza kuazima simu na kumpigia rafiki yake Chausiku aitwae Sabrina. Huyu namba yake niliweza kuihifadhi kwenye kijitabu changu kidogo na kumpa habari ya ajali, alipata mshituko kwani hakuweza kujizuia na kunambia atakuja muda sio mrefu.

Baada ya masaa mawili kutokana na umbali anakoishi Sabrina aliweza kufika pale na kunikuta hospitali nikiwa nimenyongea. Kwa bahati wale wasamaria waliweza kutuacha na tukawashukuru kwa msaada wao mkubwa walioufanya.

“Haya vipi shemeji, ilikuwaje?” Sabrina ananiuliza

Nami nikamueleza habari yote ya ajali huku macho yangu yakiwa yakiwa yana uwekundu kwa mbali nikijikaza kutokana na kulia. Ile hali ya macho yangu haikuweza kujificha kwani hata Sabrina aliiona na kunipoza pamoja na kunipa moyo.

Nikamgeukia, na kumwambia “Sabrina, Chausiku nilitokea kumpenda sana na mpaka nasikia tetesi za kutaka kuolewa niliumia zaidi na kibaya kingine alinificha.”

Baada ya kuongea hayo nikaona Sabrina kama vile kapoa na kutazama pembeni. Sikujua kwa nini, nikaendelea,

“Leo kama Mungu namuona mitaa ya Kariakoo, namuuliza lakini bado hakuning’azia, halafu ni mja mzito Sabrina. Hii ina maana alikuwa ananisaliti kipindi tuko wote? Hivi wewe ulikuwa unafahamu yote haya? Mbona hukunambia mchezo wote huu mpaka mimi nafanyiwa haya, hukunitakia mema kwa rafiki yako?”

“Sikiliza shemeji” aliongea Sabrina

“Mimi ndie rafiki yake mkubwa Chau, na kwa sasa embu tufanye kumuombea mungu kwanza jambo hili lipite. Hayo mengine yataongeleka huko mbele, … lakini…”

Wakati anaendelea, Daktari akatokea na kuita 

“Mwenye Mgonjwa wa Chausiku”

Nikasimama haraka na kumfuata Daktari, “Ni mimi hapa”

Daktari akanishika begani na kunambia “Nina habari nataka kukupa, tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu na tumepambana sana”
Daktari alinitia hofu na kunifanya nisimame vizuri kumskiliza kwa makini

“Majeruhi wetu wa kume hatunae tena, ametutoka. Ni kazi ya mungu kwani amevujia damu ndani kwa ndani, hatukuweza kufanya zaidi ya kile tulichojaaliwa. Ila Chausiku anaendelea vizuri kwani fahamu zimerudi vizuri na baadae kidogo mnaweza kwenda kumuona. Tumegundua pia alikuwa mja mzito ila uja uzito wake kwa uchunguzi wa awali unaonekana hauja athirika ila tutaendelea kumchunguza zaidi tena kujiridhisha”

Baada ya kuongea maneno yale Daktari yule aliniacha na kuendelea na majukumu yake mengine. Nilishusha pumzi nzito kama mtu aliyekuwa amebeba dunia mabegani mwake, nikamfuata Sabrina na kumpa habari zile. Sote tulishukuru mungu kwa Chausiku kuwa na afya njema na kupona mtihani ule, hivyo tukaenda nje kwa ajili ya kumuacha Chausiku aendelee kupumzika huku tukifanya jitihada za kuwapigia simu wazazi wake kwani mwenzangu Sabrina alikuwa na simu.

Tulielekea kwenye mgahawa pale pale Muhimbili ndani kwa ajili ya kupumzika huku tukisubiria Chausiku apate mapumziko kutokana na hali yake, hatimaye tukawapata wazazi wa Chausiku na kuwapa habari ile. Iliwashtua sana ila kwa kuwa walikuwa wanamfahamu Sabrina vizuri walimwambia amsimamie mpaka wao watakapofika, kwani wao walikuwa wanatokea Kibaha.

Baada ya Sabrina kuwataarifu wazazi wa Chausiku kuhusu ajali ile. Nikamgeukia na kumuuliza, “Ulikwa unataka kusema kitu kabla Daktari hajaja?”

Sabrina aliinama chini na kuanza kunielezea.

“Najua mimi sio muhusika na msemaji wa maneno haya, ila ukweli ni kwamba, Chausiku anakupenda sana wewe. Ile ndoa alilazimishwa na Baba yake kwani walikuwa hawakutaki wewe sababu ya elimu na pesa, waliona mtoto wao anateseka na wao hawafaidiki na chochote. Hivyo wakaamua kumlazimisha kuolewa na yule bwana, yule bwana anaitwa Karim ni wale wasomi waliosoma nje ya nchi, aliagiza atafutiwe mchumba na mzee ndio akalazimisha.

Chausiku hakujua hilo, ila Mzee wake alitumia ujanja wa kumuita kijijini na kumlazimisha ndoa, ndio maana kipindi kile alivyokuaga anaenda nyumbani akachelewa kurudi, ikawa hapatikani hewani kwani simu alipokonywa. Hata mimi alikuja kunipigia simu baada ya wiki tatu na kunambia ukweli ila nikashindwa kukutafuta kwani wewe nawe huna simu na pale Tandika ulipokuwa unakaa ukahama. Hivyo ikawa ngumu kukupata lakini sio kweli kama alikuwa anakusaliti na hilo swala la mimba hakuniambia chochote”

Tulikaa mpaka mida ya alasiri kwani hakuna kati yetu aliyeweza kuinua miguu yake na kuelekea kwenye shughuli nyingine, Sabrina alinieleza kinaga ubaga ni kwa kiasi gani Chausiku alikuwa hakubaliani na ile ndoa ila kwangu ilikuwa ni kama usiku wa giza kwa kipindi chote hicho. Nikajisemea moyoni 

“Ndio maana hakuweza kunijibu chochote kwa kipindi kile namuhoji kwenye gari – nilikuwa namshutumu bure”. 

Nikajiapiza kumsikiliza na kutomshambulia tena pindi atakapokuwa yuko salama. Baada ya muda kidogo, nikamshauri Sabrina twende ndani tukamuangalie Chausiku kwani ni masaa kadhaa yamepita na twaweza ruhusiwa kumuona japo kwa uchache. Tuliingia ndani na kwenda moja kwa moja maulizo kwa wauguzi na kuuliza.

Tukaelekezwa wodi alipopelekwa, tukaenda kumuona, ijapokuwa hakuwa na nguvu za kuongea sana ila aliponiona tu machozi yalimtiririka mashavuni mwake na kulia kwa uchungu.

Nikamuwahi kwa kumshika mkono na kumwambia, “Sabrina ameshanieleza yaliyokutokea kipindi chote hichi. Nisamehe mimi kwa kukushutumu ila sikuwa najua”

Chausiku alitabasamu kwa mbali ila hakuweza kunijibu chochote na akaishia kuangalia tumbo lake akiwa na wasiwasi na kiumbe kile alichobeba. Nikamsogelea kwa karibu zaidi na kumueleza,

“Daktari ametuambia uja uzito uko salama, umepata mshtuko kidogo ila wataendelea na uchunguzi zaidi hapo baadae”.

Maneno yangu yalimtia nguvu kama vile mtu aliekata kiu baada ya kukaa nacho kwa mrefu. Aliuinua mkono wangu na kuupeleka kwenye tumbo lake kisha na kuniita 

“Mashaka”

“Huu ujauzito ni wako, ilikuwa siri yangu. Kabla sijakwambia ndipo nikapigiwa simu na baba ananiita nyumbani, nikasema nikirudi nije nikushtukize ila haikuwa hivyo. Nina mengi ya kukueleza ila nilipitia mengi kwa yule bwana kwani hakuwa mume mwenye mapenzi na huruma kwangu. Alinidharau kwa kuwa ni maskini na sikusoma, niliomba Mungu kila siku anitoe kwenye mtihani ule, na sikuweza kumwambia kuhusu mimba hii kuwa sio ya kwake, alijua ni yake kwani angezidi kuninyanyasa. Siamini kama ndio wewe ulienisaidia mpaka nimefika hapa”

Nikautoa mkono wangu tumboni mwake na kumfuta machozi usoni mwake na kumwambia;

“Chausiku, siamini unachoniambia. Moyo wangu umepata mshtuko ghafla, huu uja uzito uliondoka nao kipindi kile? Ama kweli Mungu ni mkubwa, leo amenikutanisha na mwanangu. Nitakutunza Chau wangu, nitaendelea kupambana kwa kadri niwezavyo mpaka mtoto azaliwe na uwe na afya nzuri”

Baada ya kunambia maneno yale, tukamtaarifu habari ya msiba wa yule mwanaume aliyekuwa nae.

Cha ajabu Chausiku hakusikitika wala kujuta, aliishia tu kuitikia na kusema;

"Hakuna amuombeaye mwenzio kifo ila ni ahadi yake ilikuwa imefika, Mashaka - yule ndio alikuwa Karim, mume wangu nilieishi nae kwa mateso. Haikuwa kazi rahisi na ujauzito huu, ni mungu tu ndiye aliyekuwa ananisitiri, nisingependa tuendelee kuongea sana kuhusu yeye. 

Nimefurahi kukuona Mashaka, amani imerudi moyoni mwangu. Ila nahisi kuishiwa nguvu, natamani niendelee kuongea nawe"

Baada ya kusema vile tukaona mimi na Sabrina tumuache apumzike kwa uchovu alokuwa nao.

^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^
Tulikuwa tunatoka kliniki na Mama Harith huku mtoto akiwa amelala kwa kuchoka kwani tulienda kupima uzito tu na kuondoka. Chausiku alikuwa ni mama mwenye afya maridadi huku nami nikiwa nimeota kitambi kwa mbaali cha kufutia simu ya ‘touch’ – smartphone. Maisha yetu yalikuwa mazuri kwani hatimaye niliweza kumuoa Bi Chau baada ya kuwa mjane na kisheria kurithi mali za marehemu mumewe, hivyo kupitia mali zile tuliweza kufanya mapinduzi ya kimaisha baada ya kunisihi sana tuzitumie kujenga penzi letu na maisha yetu.
Kwa kuwa tulipendana sana, hali ile tukakubaliana nayo nami nikakubali kuanza maisha naye kwa uwezo ule wa kifedha alokuwa nao. Tuliweza kwenda kijijini kwa wazazi na Chausiku aliweza kutoa msimamo wake juu yangu na kutaka nimuoe kwani mie die mwanaume anitakae kimaisha na anipendae ikiwa ni pamoja na kuwa ni mzazi mwenzie. Wazazi safari hii hawakuwa na pingamizi kwani walijua kilichomtokea mtoto wao na hivyo kututaka radhi na kutuambia kwamba
“Shetani na tama zilituponza wanetu, hivyo kwa sasa sisi hatuna pingamizi. Tuko radhi na ndoa na mnaweza kuoana”
Hivyo jambo la ndoa likapita, tukapata mtaji mzuri wa kuanzisha biashara ya usambazaji maji kupitia ofisi kubwa ya uwakala tulioanzisha  na pia tuliweza kujimudu kujenga nyumba kwa ajili ya wazazi wa Chausiku  na mara kwa mara ilikuwa tukiwatembelea na kuwapelekea mjukuu wa kucheza nao na hivyo hawakuwa na namna ya kukubali na kubariki maisha yetu
MWISHO

April 14, 2018

MSEMO WA LEO: 14-04-2018

Maya Angelou
Katika safari ya maisha tunakumbana na vitu vingi kwa kuwa kila siku kuna mambo mapya, yapo uyapendayo na mengine ni kinyume. Ila tunajitahidi kuendana nayo ili tufike tunapopataka, ujanja wa kufika kiurahisi anao MAYA ANGELOU kupitia MSEMO WA LEO


"If you don't like something, change it. If you can't change it, change your attitude."
-- Maya Angelou

"Kama kuna kitu hukipendi maishani mwako, kibadilishe. Kama huwezi basi badili mtazamo wako"
-- Maya Angelou



Kwa historia ya msemaji wa leo ingia hapa:

April 14, 2018

MAGAZETINI LEO: 14-03-2018