Tuesday, 27 March 2018

Hadithi Fupi Na. 5: Pembe Cassava Products

HADITHI FUPI Na. 5
PEMBE CASSAVA PRODUCTS
MTUNZI: ISIHAKA ‘NUKTA’ KIBAO
Ilikuwa saa 10 alasiri, nyuso zote zilikuwa na huzuni zikitafakari safari ya maisha ya mwana Adamu. Huwa hamna lolote, si majigambo wala ukubwa wa mtu, nguvu zake, utajiri, wala umaarufu. Sote safari yetu ni moja, akhera, na kila mtu atapitia mlango wa umauti. Kama sheikh alivyokuwa akimalizia mawaidha pale makaburini ya kuwa kila nafsi itaonja umauti na kwa Mwenyezi tutarejea.

Msafiri, alikuwa rafiki yangu niliyesoma nae shule ya msingi na kupotezana nae kwa muda mrefu, ila kama bahati tu tulikuja kukutana ikiwa mimi nipo kwenye harakati za kutafuta ajira ndipo urafiki wetu ukarudi kwa kasi kwani yalipita mengi na tulikuwa na mengi ya kufanya ili tuyajenge maisha kupitia mipango ya miradi tuiyoiweka. Msafiri alikuwa msomi wa kiwango cha degree, tofauti na mie nilieishia kidato cha nne na kusomea udereva. Ila ilikuwa kazi ya mungu na hatimaye ametangulia mbele ya haki na kuniacha njiani. Nilijiskia uchungu kwa kuwa alikuwa rafiki na mwenzangu kwenye mipango tuliopanga.

Baada ya mazishi watu walitawanyika wakiwamo Baba Mzazi wa Msafiri, nilimfuata na kumpa pole yake na kumsihi kuwa mvumilivu kwenye kipindi hiki kigumu. Alinitazama usoni na kunishukuru ila hakuweza kunitambua kwa haraka kama tulikuwa tukicheza wote na mwanawe kipindi tuko wadogo nyumbani kwake. Ila sikutaka kumkumbushia maana haukuwa muda muafaka. Nilitoka maeneo yale ya makaburi ya Kinondoni na kuelekea nyumbani Gongo la Mboto huku nikifikiria nafanyaje mipango ile kwani Msafiri kwa kiasi kikubwa ndio alikuwa mtoaji hela kwenye mipango yetu.

Nililala huku nikiwaza nitafanyaje niweze kuboresha maisha yangu kwani hata ajira niliyokuwa nayo nilishikwa mkono na kuwekwa kwa mchango wa Msafiri. Sasa ameshafariki, isije ikawa ameondoka na nia za watu kutaka niendelee kuwepo kazini, nilipiga moyo konde na kuendelea na kazi. Kulipokucha nilidamka kama kawaida na kuelekea kazini, niliwahi sana kuliko siku zote hadi mlinzi wa ofisini akanishangaa na kuniuliza

“Leo kulikoni?”

Nikamjibu, “Jana sikulala vizuri kwani nilikuwa natafakari mengi”

Yule mlinzi alinielewa kwani tulikuwa marafiki wa karibu kiasi chake. Hivyo akanipa moyo na kunieleza nisiwaze sana wala kukata tama na niendelee kupiga kazi kwani mtoaji riziki ni Mwenyezi pekee.

Mazingira yangu ya kazini kiukweli hayakuwa endelevu kwani kila siku zilivyokuwa zikiyoyoma mahusiano na wafanyakazi wenzangu yalikuwa yakipungua taratibu kama mwendo wa kuzama jua. Nililiona mapema, kwa kuwa ofisi ilikuwa ni ya watu asili ya bara Asia, hivyo alikuwa anaandaliwa mtu wa kuchukua nafasi yangu.

Hatimaye baada ya miezi mitatu nikaja kupewa barua ya kuwa ofisi inataka ipunguze baadhi ya wafanyakazi kwani gharama za uendeshaji zimekuwa kubwa na hivyo ikanibidi mimi niwe mmoja kati ya wanaotakiwa kuondoka katika nafasi ile. Siku nakabidhiwa ile barua, moyoni mwangu sikujaa hofu kwani nililitarajia lile na nilikuwa nikiomba mungu aniandalie mazingira mapema ya kujikwamua kiuchumi, kwa hivyo nikawa katika mtihani wa subira maana kwengine kote kulikuwa hakuna mang’azo.

Niliipokea barua, nikapumzika na kazi ile ila nisingependa kuitaja ofisi kwa jina. Nilipitia kipindi kigumu sana katika maisha yangu kwani ilifikia kipindi ilikuwa sina hata nauli ya kuja mjini kutafuta kazi kutokea kwangu Gongo La Mboto. Kwa bahati, nilikuwa nimelipa kodi ya mwaka mzima kwa msaada wa Msafiri, aliniongezea fedha kidogo katika chumba nilichokuwa nakaa, hivyo pakuweka ubavu nilikuwa napo kwa muda. Ilipita miezi saba, kula yangu ya mashaka, sikuweza kununua hata nguo wala viatu vipya na michango yote ya kijamii ikiwamo harusi, misiba na mengineyo watu waliniona mchungu. Ilikuwa nafanya vibarua tu na “Udeiwaka kwenye magari”

Ndipo siku moja nilikuwa natokea zangu Ukonga narejea nyumbani, katika katika pita pita zangu kwa mguu nikaamua kwenda kibanda cha magazeti, naikumbuka siku hii kwani pale ndipo nilipopata msingi wa mabadiliko ya maisha yangu na mpaka kuwa hivi nilivyo. Nilikuwa sina hela ya kununua gazeti, hivyo nikapitia vichwa vya habari magazetini na nikaishia kuondoka, wakati naondoka eneo lile likanipita basi la abiria likiwa linaelekea Chanika likitokeaaaa…. Buguruni kama sikosei. Lile basi lilikuwa linakwenda kwa mwendo wa taratibu huku likivizia abiria kwani wengi ilionekana walishuka pale Ukonga.

Nikalitazama kwa makini huku likiendelea na safari yake, kwa nyuma ya lile basi nikaona msemo umewekwa “Lipo linaloshindikana Chini ya Jua – Kupiku ufanisi wangu”. Ule msemo ulinishangaza na kunishtua, nikatabasamu kwani niliona ni ubunifu wa maneno tu. Lakini wakati naendelea na safari yangu, ule msemo ukanirejelea kichani na kunifikirisha kidogo, hivyo nikawa najiuliza. Yulemwandishi alimaanisha nini? Chini ya jua… ufanisi… nilitafakari kwa muda na kuja kugundua kuwa unapokuwa mahiri kwenye jambo Fulani na ukalifanya kwa ufanisi basi hakuna atakaeweza kufanya kama wewe.

Aaaah! Nikamkumbuka Msafiri rafiki yangu, nikatembea haraka haraka hadi kufika nyumbani na kufungua yale makaratasi tuliyo andaa kwenye mikakati yetu na kugundua kuwa, mipango yote ilikuwa mimi ndio mtendaji mkuu maana wazo la biashara yetu nililitoa mimi kutokana na uzoefu wangu wa biashara ile, Msafiri alikuwa ni mtoaji mtaji mkuu pamoja na kujitolea baada ya muda Fulani kwani biashara za usafirishaji alikuwa hazifahamu kabisa.

Niliamua kupitia upya ule mpango mkakati na kutafakari nitapataje mtaji wa kuanza biashara ile. Likanijia wazo la mkopo kwenye taasisi za fedha lakini halikuwa wazo zuri kwani ndio nilikuwa naanza biashara hivyo ingekuwa hatari kwangu, nikaangalia nani wa kumfuata ili aweze kunikopesha fedha, ila pia ilikuwa ngumu kwa maana kila niliemfuata aliniona ni mtu ambaye sina uhakika wa kurudisha zile fedha. Hivyo ikanichukua muda mrefu kiasi nikafikiria kuachana nalo tena lile wazo.

Siku moja jioni nikiwa nimekaa, likanijia wazo jingine, nikajisemea kwa nini nisimfuate Baba yake Msafiri nimuelezee nini tulipanga na mwanae na tulifikia wapi, ila akili nyingine ikawa inapingana na wazo lile kwani isije ikawa Mzee anaona nataka kutumia jina la mwanae kupata fedha kutoka kwake, na nikiangalia hata mwaka haujatimia toka mwanae afariki. Lakini nikapiga moyo konde nikasema nitamfuata kwani mguu wa kutoka Mungu huutia Baraka.

Asubuhi yake  nikatoka na kuelekea nyumbani kwa Mzee wake Msafiri, nilipofika haikuwa kazi rahisi kwani niliona vigumu mwanzoni kumuelezea ila nikawa sina budi na kumueleza ya kuwa mimi na mwanawe tulipanga kufanya biashara ya usafirishaji bidhaa, tukianza na mchele kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam na kisha kusafirisha mihogo kutoka Tanga kuja Dar es Salaam. Ila tulikuwa hatuna usafiri wa kwetu wala ofisi ya biashara, na kwa kiasi kikubwa mtaji aliahidi kutoa Msafiri ili nami niingize nguvu kazi kwani nina uzoefu wa mambo ya usafirishaji.

Nakumbuka Mzee wangu huyu aliniuliza, kwa nini tulitaka kufanya biashara ile. Nami nikamjibu, kujikwamua kiuchumi na hatimaye kuwa na kitu cha kwetu cha kujivunia kitakacho tuwezesha kusema “Sisi tumefanikisha haya, na tunamiliki hiki na hiki”. Mzee alinisikiliza kwa makini melezo ya biashara ile na alivutiwa sana kwa vile tulivyokuwa tumepangilia ile biashara na vile itakavyokuwa inaenda. Baada ya kumaliza kumuelezea mchanganuo wa biashara, alitabasamu na kunifanya nijiskie kama mtu aliepumzika kivulini kutokana na kupigwa na jua kali na kuhisi kuna matumaini.

Akanambia, sikiliza mwanangu ‘Mimi ni kama Mzee wako, ulivyonikumbusha kipindi mnacheza wote na mwanangu kipindi wadogo nikakumbuka vitu vingi kuhusu mwanangu. Na kama ndoto hii mwanangu alitaka kuitimiza, mimi nitakusaidia kwani nafahamu hata yeye atafurahia huko alipo’. Nakumbuka pia aliwahi kunigusia kutaka kuanzisha biashara ila hakunieleza kinaga ubaga kutokana na safari zangu kikazi. Mzee akaniahidi kunipa mtaji wa milioni 3 ili nianze biashara ya kusafirisha mihogo kutoka Mapojoni, Tanga na kunambia kule Tanga pia ana marafiki zake ataniunganisha nao ili biashara iende kwa uhakika.

Nilitabasamu na kumshukuru sana Mzee kwa shukrani zote kwani alikuwa amempiga teke chura, na nikamuahidi sitomuangusha kwa mchango wake ule. Zilipita siku kadhaa, akanikabidhi mtaji ule, nikawasiliana na marafiki zake wa Tanga kupitia jina lake, wakawa wananikusanyia mzigo namimi kuupokea Dar es Salaam kwa kuusambaza. Biashara ilikuwa ya mafanikio makubwa sana kwani niliweza kuchukua mzigo mwingi na hatimaye kuwa na usafiri wangu wa kuchukulia mzigo Tanga, nikamiliki ofisi ya usambazaji na mwisho nami nikaajiri watu wawili.

Nimefikia hapa, ni miaka mitatu sasa ambayo ni ya mapito aina mbali mbali lakini kitu kilichokuwa kinanipeleka mbele kwanza ni ule msemo “Lipo linachoshindikana chini ya jua – kupiku ufanisi wangu” kwani nilijitahidi kwa hali na mali kuhakikisha nabaki kwenye biashara na nazidi kukuwa kimafanikio, Baba yake Msafiri yeye ndiye alikuwa ufunguo wa safari yangu hii, kwani ukiachilia mbali kunichukulia kama mwanawe, aliniamini na kuthubutu kuweka pesa yake kwenye biashara hii nami sikumuangusha kwani amejionea ninachofanya na mpaka sasa amekuwa mdau mkubwa na msimamizi mkuu wa PEMBE CASSAVA PRODUCTS.

Mpaka nafungua kiwanda cha kati na kati kiuzalishaji ni mashauri yake Baba Msafiri na hekima zake juu ya uendeshaji wa biashara na usimamizi. Hakuniacha Mzee wangu huyu nami bado naendelea kuchota hekima kutoka kwake. Mafanikio niliyoyapata kuanzia kumiliki usafiri wa biashara, usafiri binafsi, kuwa na makazi nyumbani hadi kujenga familia ni chachu iliyotokana na biashara hii na Mzee wangu huyu.

Hivyo ningependa niwashukuru kwa kusikiliza historia yangu kwa ufupi naamini itaweza kushawishi vijana wenzangu na jamii kwa ujumla. Mwisho ningependa muendelee kutumia bidhaa za PEMBE CASSAVA PRODUCTS kwani ni bidhaa bora sokoni, kuanzia unga wa muhogo, mihogo, na  miche kwa ajili ya kupandia.

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

“Naam, huyo ndio bwana Mwinyipembe Mzava, Mjasiri Wa Mali wetu wa leo, umekuwa ni mshawishi mkubwa kwa vijana na kwa hakika umetuletea mapinduzi ya kifikra na kiuthubutu, kwani historia yako itawaathiri watu wengi leo”

Aliongea Fatime, mtangazaji wa Nukta FM, radio ya Tanga. Aliongeza, “Tunakushukuru Bwana Mwinyipembe kwa kuwasili kwenye kituo chetu cha radio Nukta FM na kuridhia kuelezea historia yako ya maisha tokea ulipoanzia mpaka hapa ulipo. Kwani ni kijana mwenye mafanikio ya kuigwa na tunaamini utaendelea kushawishi wengine kwa vitendo na maneno, taifa letu linahitaji kujua watu kama nyie mlianza vipi na mlipita pita vipi ili watu wapate funzo na wachukue hatua. Hilo ndio lengo kuu la kipindi chetu cha MJASIRI WA MALI.”

Baada ya hapo Fatime alimalizia kwa maneno machache

“Nawashkuru watu wote waliotega sikio kwenye kipindi chetu cha leo na kusikiliza historia fupi ya Msajiri Wa Mali Bwana Mwinyipembe, kwani naamini tumejifunza mengi na tuendelee kupambana. Unapokuwa na wazo lako usikae nalo tu, jaribu kutafuta nani wa kumfuata ili uweze kuwezeshwa kwa namna moja au nyingine. Endeleeni kusikiliza Nukta FM kwa vipindi vijavyo, endelea kutega sikio”

Fatime alinigeukia na kunipa mkono wa shukrani kwa kuwasili kwenye kipindi kile kwani niliweza kushawishi wachangiaji wengi kupitia ujumbe mfupi wakati wa mahojiano yale, na wengi walikuwa vijana wakitaka tuonane kwa ajili mashauri ya biashara. Tuliagana na Fatime nami nikaweza kuchukua usafiri wangu ambao nilikuwa nimeenda nao na kuelekea nyumbani kwa nilikuwa nahisi njaa na nilipofika nilimkuta mke wangu kashaniandalia chakula kwa ajili ya kula.

MWISHO

No comments:

Post a Comment