JINA: MUDA WA KIFO NI SAA MOJA NANUSU
Mtunzi: Isihaka "Nukta" Kibao
Mtunzi: Isihaka "Nukta" Kibao
Nilikuwa napiga
hatua kidogo kidogo huku nikiwa sijali vumbi wala vijiwe jiwe vilivyokuwa
vinaniumiza wakati nikivikanyaga huku viatu vyangu vikichafuka kwa vumbi la
mwendo mrefu, pamoja na fujo za mtaa ule za watoto kucheza mpira wa miguu huku wakiwa
wamechimbia miti ardhini kama magoli, wanawake upande wa pili wakiwa
wamejikusanya wakisukana wakiwaonya wale watoto kutowapiga na mpira, wengine
wakiendesha baiskeli kwa kufanya njonjo lakini akili yangu yote haikuwa katika
mazingira yale.
Kilichokuwa
akilini mwangu ilikuwa ni mawazo ya harusi ya msichana Belinda. Kwanini imepita
kwa mtindo ule, na kwanini alinifanyia vile? Nilijiona ni kiumbe nisiye na
thamani pale mjini. Mtaa ule wa fujo niliweza kuupita kwa huruma ya Mungu
kutokana na fujo zake kwani nilikuwa mfano wa kivuli kiasi watu kutonijali wala
kunigonga na aidha mpira au baiskeli za watoto.
Baada ya kuuvuka
mtaa ule salama salmini nikamkumbuka Shukuru ambaye alikuwa ni kaka wa Belinda.
Nikaingiza mkono mfukoni na kutoa simu ili nimpigie, kwani yeye ndiye angeweza
kunipa maelezo stahiki ya harusi ile. Mara ghafla nikaona gari imepita kwa kasi
huku ikiuelekea mtaa ule wa fujo. Nikajiuliza ni nani awezaye kuendesha kwa fujo
namna ile kwenye mitaa iliyojaa watu, haikupita dakika moja nikaskia kishindo na
makelele ya akina mama. Mawazo yote yakaniruka na ikanibidi kuelekea kwenye
eneo la tukio kushuhudia nini kinaendelea.
Kwa kuwa sikuwa mbali
nikafika pale mara moja na kuona watoto na wale akina mama wamezungukia kitu
katikati, akili yangu ikanipa ni ile gari imesababisha ajali mahala pale. Sikuwa
mbali na ukweli kwani ilikuwa ajali na mtoto wakiume mmoja alikuwa amegongwa. Baada
ya kuona vile nikafanya haraka kuingia katikati ya kundi lile na kutoa msaada
kwa kumpatia yule mtoto huduma ya kwanza na kuwaamuru wasogee mbali kidogo ili
mgonjwa apate hewa safi kwani alikuwa amelala chali na damu zikimtoka upande wa
sikio la kushoto.
Kuangalia kwa
pembeni, aliyesababisha ile ajali alikuwa ni kijana mdogo ambaye alikuwa
ameshikwa na butwaa asijue la kufanya, maana watu walimzonga huku wakimzogoa. Mara
akatokea mtu mzima mmoja wa kiume ambaye alijulikana kuwa ndiye mzazi wa yule
mtoto, akiwa na wasiwasi mkubwa juu ya hali ya mwanae. Ndipo nikamueleza kuwa
Mimi ni Dokta na yambidi afanye haraka kumuwahisha mtoto hospitali. Yule aliyesababisha
ajali ikambidi abebe jukumu la kumpeleka mtoto hospitali, nami baada ya kuona
hali ile ikanibidi niingie garini ili nikatoe msaada zaidi.
Tulifika Hospitali
ya Rufaa ya Bombo (Tanga) saa moja na dakika tano usiku. Nami nilivyoingia
pale, muuguzi Maria baada ya kuniona tu akanisalimu
“Dr. Kera,
kwema? Mbona umerudi uko hai hai…”
Nikamwambia
“Nina mgonjwa na
yambidi niingie nae chumba cha watu mahututi”
Hivyo akafuatilia
kitanda mara moja cha kumbebea mtoto yule, huku mimi nikienda chumba cha
madaktari kujiandaa ili kuokoa maisha ya mtoto yule. Tunaingia chumba cha watu
mahututi ni saa moja na dakika ishirini na tano.
Tunaanza uchunguzi
wa mgonjwa yule, kitu cha kwanza tunagundua damu nyingi zimemtoka sikioni na
kwa upande wa uchogoni inaonekana kuna ubonyeo kana kwamba alijipigiza na
uchogo alivyoanguka. Baada ya uchunguzi huo wa awali, namwagizia mhudumu Rukia
alete mashine ya kupumulia ndipo tunagundua mgonjwa wetu yule hapumui tena
kwani mashine ile haikufanya kazi, anakata pumzi na kufariki.
Tukafanya juhudi
zetu za kumuokoa kwa kuushtua moyo na kumsugua kifuani ila haikufaa. Baada ya
kuona vile nikarudi hatua moja nyuma na kuangalia saa, nikaona ni saa moja na
nusu.
Nikafikiria itakuwa
ngumu kiasi gani kwa mzazi wake kumpa habari ile, ila nikapiga moyo konde kwani
madaktari ni sehemu ya kazi yetu kutoa habari za msiba kwa wahusika na
nikafanya hivyo. Nikamueleza baba wa mtoto habari ile na niliushuhudia uchungu
wa mtoto kwa mzazi ila ndio ilikuwa kazi ya Mungu.
Baada ya pale
nikaona nijiwekeze zaidi kwenye kazi yangu na kuachana na habari ya Belinda
kwani usaliti alonifanyia haukuwa wa kawaida kuchukuliwa na rafiki yangu wa
karibu kipindi niko masomoni nje ya nchi.
MWISHO.
KWA HADITHI NYINGINE TAFADHALI INGIA HAPA;
No comments:
Post a Comment